Chanzo cha picha, Carolyne Odour
-
- Author, Anita Nkonge
- Nafasi, BBC News Nairobi
Carolyne Odour ameiambia BBC kuwa anahofia sana hatima ya wanawe wawili wadogo ambao walitoweka miezi miwili iliyopita na baba yao – mfuasi wa mafundisho ya kiongozi mashuhuri wa ibada ya njaa.
Bi Odour anasema kuwa huku kukiwa na uchunguzi unaoendelea kuhusu vifo zaidi vinavyohusiana na ibada hiyo ameutambua mwili wa mumewe katika chumba cha kuhifadhia maiti mjini Malindi pwani ya Kenya.
Maiti yake ilipatikana mnamo mwezi wa Julai katika kijiji cha Kwa Binzaro, viungani mwa Malindi na karibu na msitu wa Shakahola, ambapo zaidi ya miili 400 ilipatikana mnamo 2023 katika mojawapo ya visa vibaya zaidi kuwahi kutokea vya vifo vya watu wengi vinavyohusiana na ibada.
Bi Odour sasa anasubiri matokeo ya vipimo vya viini vya vinasaba yaani DNA vinavyofanywa kwa zaidi ya miili 30 iliyogunduliwa hivi karibuni.
“Nilihisi maumivu. Nilimtambua kwa shida. Mwili wake ulikuwa ukioza vibaya,” Bi Oduor, 40, alisema kuhusu mumewe Samuel Owino Owoyo.
Anaamini wanawe, Daniel mwenye umri wa miaka 12 na Elijah wa miaka tisa, walisafiri na baba yao mwenye umri wa miaka 45 kwenda Kwa Binzaro mwishoni mwa Juni.
Mchungaji anayejitangaza Paul Mackenzie kwa sasa anashtakiwa kwa kile kinachoitwa “Mauaji ya Msitu wa Shakahola” – na amekana kosa la kuua bila kukusudia.
Anadaiwa kuwaambia wafuasi wake wangefika mbinguni haraka zaidi ikiwa wataacha kula – na kumekuwa na wasiwasi kwamba amekuwa akiwasiliana na wafuasi wake kutoka jela.
Bi Odour anasema mumewe alianza kusikiliza mafundisho ya Bw Mackenzie miaka minne au mitano iliyopita.
“Alibadilika na hakutaka watoto waende shule,” alisema. “Wakati watoto walipougua alisema kwamba Mungu atawaponya. Aliamini sana mafundisho hayo.”
Kubadilika kwa maoni yake kuhusu elimu rasmi na uingiliaji wa matibabu kulisababisha kutoelewana kati ya wanandoa hao, ambao walikuwa na watoto sita pamoja nyumbani kwao huko Mudulusia katika kaunti ya Busia, magharibi mwa Kenya, karibu na Ziwa Victoria.
“Mafundisho hayakuwa na maana kwangu,” Bi Oduor alisema. “Mtoto anapokuwa mgonjwa, ndio ninaamini Mungu anaweza kuwaponya, lakini pia najua kwamba mtoto anapokuwa mgonjwa unampeleka hospitalini.”
Miezi miwili iliyopita mnamo 28 Juni, hali ilibadilika kuwa mbaya wakati mumewe aliondoka na wana wao wawili wadogo.
“Aliniambia alikuwa akienda katika kijiji [cha kuzaliwa],” Bi Oduor alisema. “Simu ya mwisho tuliyopata aliniambia, ‘Tumekwenda, Mungu awe nawe.’ Na nikamwambia, ‘Kuwa na safari salama.'”
Lakini Bi Odour alianza kushuku wakati hakuwasiliana naye tena.
Baadaye aligundua kuwa hakuwa ameenda katika kijiji cha wazazi wake katika kaunti ya Homa Bay, ambayo pia iko karibu na Ziwa Victoria, karibu kilomita 200 (maili 125) kusini mwa Mudulusia.
Akifuatilia hatua zake, aligundua kwamba alikuwa amepanda basi kutoka nyumbani kwao katika kaunti ya Busia na kusafiri na wavulana hao zaidi ya kilomita 900 mashariki hadi Kwa Binzaro katika kaunti ya Kilifi nchini Kenya.
Aliwajulisha polisi na kutoa habari haraka kupitia mitandao anuwai katika jaribio la kuwapata.
Wiki chache zilizopita alipigiwa simu akisema mtu ambaye anafanana na jinsi anavyomuelezea mumewe alikuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Malindi.
Bi Odour alisafiri kwenda eneo la pwani mnamo 19 Agosti kuthibitisha kifo cha mumewe.
Aliambiwa mwili wake ulipatikana katika kijiji cha Kwa Binzaro mnamo Julai 19 wakati wa uvamizi wa polisi ulioandaliwa kwa sababu ya ripoti za kutoweka kwa tuhuma.
Polisi walisema alikuwa amegunduliwa kwenye vichaka karibu na nyumba inayoshukiwa kuhusishwa na ibada ya kufunga hadi kufa na alionekana kuwa alifariki kwa kunyongwa.
Inadaiwa kuwa baadhi ya waathiriwa wa mauaji hayo walinyongwa walipoonekana kuchukua mrefu kufa kwa njaa.
Kufuatia uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma nchini Kenya, watu 11 walikamatwa kuhusiana na kesi hiyo, wakiwemo watatu ambao walikuwa wafuasi wa Bw Mackenzie.
Utafutaji wa miili zaidi ulianza tarehe 21 Agosti. Kufikia sasa, miili 32 imefukuliwa na zaidi ya sehemu 70 za mwili zimepatikana zikiwa zimetawanyika msituni.
Kwa Bi Oduor, imekuwa mchakato wa kutisha kushuhudia.
“Unaona miili ikifukuliwa, na hata hujui hali ya watoto wako mwenyewe,” alisema. “Inaumiza sana.”
Dk Raymond Omollo, mtumishi mwandamizi wa serikali katika Wizara ya Mambo ya Ndani, aliiambia BBC kwamba serikali inakusudia kuanzisha sheria kali za kukabiliana na misimamo mikali ya kidini na itikadi kali nchini.
“Tunafanyia kazi muswada, muswada wa kidini, ili kuweza angalau kuwa na vigezo fulani vya shirika la kidini – je ina katiba? Viongozi ni akina nani? Wana sifa za aina gani?” alisema.
Anaamini hii itasaidia kuhakikisha vikundi kama hivyo vinawajibika zaidi.
Uchunguzi karibu na Kwa Binzaro umesimamishwa kwa muda wakati wataalam wa mauaji na uchunguzi wakijiandaa kuchunguza mabaki yaliyopatikana hadi sasa.
Kwa wakaazi wa eneo hilo, uchunguzi wa hivi karibuni haujawashtua tu bali umefanya maisha kuwa magumu kwani msitu ni rasilimali muhimu kwao.
“Tunategemea msitu kwa kuni na mkaa,” George Konde, kutoka Kwa Binzaro, aliiambia BBC. “Sasa kwa sababu ya kile kilichotokea hawakuruhusiwa kuingia. Wanahitaji kusaka msitu mzima na kukomesha ibada hizi mara moja na kwa wote.”
Bi Odour anaendelea na kusubiri kwake kwa uchungu kujua waliko wanawe wawili.
“Nilikuwa nikitarajia mmoja wa wanangu kwenda darasa la 7 na mwingine darasa la 4,” alisema. “Kila wakati ninapomwona mtoto amevaa sare ninahisi maumivu kwa sababu ya kutokuwepo kwake. Sijui wanaendeleaje.”
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi