Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Mauaji ya Kimbari, chombo kinachoongoza katika suala hili na wataalam wake wakuu, wamepitisha azimio siku ya Jumatatu, Septemba 1, na kuthibitisha kwamba hatua za Israel huko Gaza zimekidhi vigezo vyote vya kisheria vya kuamua mauaji ya halaiki. Serikali ya Israel imejibu kwa kueleza taarifa ya chama hicho kuwa ya aibu, kwani imetumia vigezo vilivyotumika kuhukumu mauaji ya Holocaust.

Imechapishwa:

Dakika 4 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

“Sera na hatua za Israel huko Gaza zinakidhi ufafanuzi wa kisheria wa mauaji ya halaiki kama ilivyo katika Ibara ya II ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari (1948),” linasema azimio hilo, likiungwa mkono na 86% ya wapiga kura wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Mauaji ya Kimbari (IAGS).

IAGS ni chama kikubwa zaidi cha kitaaluma duniani cha wasomi wa mauaji ya halaiki na inajumuisha wataalam kadhaa wa Holocaust. Ina wanachama 500.

“Hii ni kauli ya uhakika ya wataalamu katika uwanja wa tafiti za mauaji ya halaiki kwamba kinachotokea kwa sasa Gaza ni mauaji ya halaiki,” mkuu wa chama hicho, Melanie O’Brien, profesa wa sheria za kimataifa aliyebobea katika mauaji ya halaiki katika Chuo Kikuu cha Australia Magharibi, ameliambia shirika la habari la Reuters.

Katika muhtasari wa sera na hatua za Israel, taarifa hiyo inaangazia mashambulizi yaliyoenea dhidi ya wafanyakazi na vifaa muhimu kwa maisha, haswa katika sekta ya afya, misaada na elimu. Miongoni mwa mambo mengine mengi, inabainisha watoto 50,000 waliouawa au kujeruhiwa na Israel, kama ilivyoangaziwa na UNICEF. Yote haya yanaathiri uwezo wa Wapalestina huko Gaza kuishi kama kundi na kuzaliwa upya.

Azimio hilo pia linasisitiza uungaji mkono wa uongozi wa Israel kwa kuwatimua kwa lazima Wapalestina wote kutoka Gaza, pamoja na hatu ya Israel ya kubomoa karibu nyumba zote katika eneo hilo.

IAGS inabainisha matamshi ya viongozi wa Israel ya kuwadhalilisha Wapalestina huko Gaza, na kuwaita wote maadui, pamoja na ahadi za “kuifuta Gaza” na kuifanya “eneo lisilo na watu.”

Majibu ya Israel yamelenga sio tu Hamas, bali Gaza yote, kwa mujibu wa chama hicho

Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imeita kauli hii kuwa ya aibu na “ikiegemea kabisa kwenye kampeni ya uwongo ya Hamas.” Israel imekanusha vikali huko nyuma kwamba vitendo vyake katika Ukanda wa Gaza vinajumuisha mauaji ya halaiki na kwa sasa inapinga malalamiko ya mauaji ya halaiki iliyowasilishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko Hague.

Watafiti wa IAGS wanabainisha kwamba kama shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023, lenyewe ni “uhalifu wa kimataifa” , jibu la Israel lililenga sio tu Hamas, lakini wakazi wote wa Gaza.

Mkataba wa mwaka 1948 wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari, uliopitishwa ili kuzuia uhalifu uliofanywa na utawala wa Kinazi wa Ujerumani usirudiwe tena, unafafanua mauaji ya halaiki kuwa vitendo vilivyofanywa “kwa nia ya kuangamiza, kwa ujumla au kwa sehemu, kundi la watu, kufuatia ukabila, rangi, au dini, kama hivyo.”

Vitendo vinavyojumuisha mauaji ya halaiki ni pamoja na mauaji ya wanachama wa kundi fulani, na kusababisha madhara makubwa ya mwili au kiakili kwa wanachama wa kundi hilo, kwa makusudi kuathiri hali ya maisha ya kundi iliyohesabiwa kuleta uharibifu wake wa kimwili kwa ujumla au sehemu, hatua zinazokusudiwa kuzuia kuzaliwa ndani ya kundi, au uhamisho wa watoto kwa makundi mengine.

Mashirika kadhaa mashuhuri ya haki za binadamu yakiwemo mashirika mawili ya Israel pia yameeleza imani yao kuwa Israel inafanya mauaji ya halaiki.

Wito wa “kukomesha mara moja vitendo vyote vinavyojumuisha mauaji ya kimbari”

“Msimamo huu wa kifahari wa kisayansi unaimarisha ushahidi ulioandikwa na ukweli uliowasilishwa mbele ya mahakama za kimataifa,” amesema Ismail al-Thawabta, mkurugenzi wa ofisi ya habari ya Hamas huko Gaza. Azimio hilo “linaweka kwa jumuiya ya kimataifa wajibu wa kisheria na kimaadili kuchukua hatua za haraka kukomesha uhalifu huu, kulinda raia, na kuwawajibisha viongozi wanaokalia kimabavu,” ameongeza.

Azimio hilo la kurasa tatu linaitaka Israel “kusitisha mara moja vitendo vyote vinavyojumuisha mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu dhidi ya Wapalestina huko Gaza, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya makusudi na mauaji ya raia wakiwemo watoto; njaa; kunyimwa misaada ya kibinadamu, maji, mafuta, na mambo mengine muhimu kwa ajili ya maisha ya watu; ukatili wa kijinsia na uzazi; na kulazimisha watu kuhama.”

Chama cha Wanazuoni wa Mauaji ya Kimbari kimepitisha maazimio tisa yanayotambua matukio ya kihistoria au yanayoendelea kama mauaji ya halaiki tangu kuundwa kwake mwaka wa 1994.

Taifa la Israel lilianzisha mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba 2023, kulipiza kisasi shambulio lililoongozwa na Hamas katika ardhi ya Israel kutoka eneo la Palestina, ambalo lilisababisha vifo vya watu 1,200 na zaidi ya mateka 250. Tangu wakati huo, mashambulizi ya kijeshi ya Israel yameua takriban watu 63,557 huko Gaza, kuharibu au kutekelteza majengo mengi ya eneo hilo, na kuwalazimu karibu wakaazi wote kukimbia makazi yao angalau mara moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *