-
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC, Nairobi
Florence Amunga ni mama wa makamo ambaye leo anatupambia Waridi wa BBC.
Simulizi ya Amunga inaanza akiwa na umri mdogo wakati ambapo alilazimika kufanyakazi ya nyumba kama yaya.
“Mimi nilianza kufanya kazi ya nyumbani nikiwa na umri wa miaka minane,” Amunga anasema.
Onyo: Baadhi ya maudhui yanahuzunisha
Mama huyo hakupata fursa ya kwenda shuleni kwa sababu mama yake mzazi hakuwa na uwezo na pia baba yake aliaga dunia akiwa na umri mdogo sana.
Akiwa kwa mwajiri wake wa kwanza, Amunga anasema maisha yalikuwa magumu kwa sababu alishindwa kutekeleza majukumu yake kama yaya.
“Sikuwa ninajua kufanya kazi, nikienda kumfanyia mtu ananipiga kwa sababu sikuweza kuosha nguo vizuri zitakate kwa kuwa umri wangu pia ulikuwa mdogo,” Amunga anaelezea.
Amunga alipitia mateso katika nyumba ya kwanza kama mjakazi kiasi cha kuchapwa na mwajiri wake ambaye alikuwa anamlipa shilingi 100 kwa mwezi.
“Ukiniangalia mwili wangu ulikuwa umebadilika, nilikuwa mweusi kwasababu ya kuchapwa na hapo ndipo nilikataa kazi kabisa na nikasema nirudishwe nyumbani, lakini mama yangu alinilazimisha kurejea kazini ili apate ile mia moja”.
Ila alipochoka, Amunga aliamua kuondoka hata ingawa hakujua anakokwenda na hatua hiyo ikawa kinyuma na matakwa ya mama yake.
Muda si muda, mama yake alimtafutia sehemu nyingine ya kufanyakazi kama yaya. Lakini anachosema Florence ni kwamba, mateso yaliendelea.
Aliamua kutoka kijijini kwenda Nairobi kutafuta maisha akiwa na matumaini kwamba yangekuwa na afueni kidogo.
“Nilishikana na wasichana wengine tukaamua kuja pamoja Nairobi kutafuta maisha kwa Waarabu”.
Ingawa pamoja na wenzake wengine ndoto yao ya kufanyakazi kwa Waarabu ilifanikiwa, kwa Florence bado mateso yalikuwa ni yale yale, sawa na kuruka mkojo na kuangukia kinyesi.
Kwa mwarabu Florence alipewa jukumu la kulea mtoto huku wengine walioajiriwa naye, wakishughulika na majukumu mengine ya nyumbani. Mwajiri wake huyo hakuwahi kumchapa, ila alimkera kwa maneno makali na kumuomba dereva wake amchape viboko pale alipoosha nguo vibaya. Mwisho wa siku aliamua kuondoka.
Wakati yuko katika njia panda, hajui pa kwenda tena na safari hii yuko mjini, ndipo alipokutana na dada ya mama yake kwa bahati, akamchukua hadi kwake.
Wakati huo akiwa na wingi wa matumaini kuwa angalau sasa amekutana na mwanafamilia, maisha yake mjini yatabadilika. Lakini hakika, safari ya mja hupangwa na Mungu.
“Nilidhani kwa vile ni dada ya mama yangu nitasaidika lakini nikageuka kuwa ninayefanya kila kitu katika nyumba yake. Nalipa nyumba kila mwisho wa mwezi wakati huo nikiwa na nguo moja pekee ya kuvaa. Nikawa naamka asubuhi kwenda kugonga milango ya wenyewe nikitafuta kazi”, Amunga anakumbuka.
Hapo ndipo aliamua kushikana na kundi la wasichana wengine waliokuja mjini Nairobi kutafuta maisha na wakamshawishi kutoka nae wakati wanaenda kutafuta kazi.
“Tulikuwa tunarauka pamoja, tunatafuta kazi, nikipata ya hoteli naanza kuwasha jiko, nabandika chai haraka haraka kisha nafagia,” Amunga anasema.
Mwanamke huyo alikuwa anazunguka kwenye migahawa akijitafutia riziki na hapo ndipo alipopatana na mvulana aliyeonyesha nia ya kutaka kuwa naye maishani.
Amunga, hakufikiria mara mbili. Moyoni mwake alijua amepata mwenza wake ambaye wataishi naye hadi kifo kiwatenganishe na wakaanza maisha yao kama mke na mume na kujaaliwa watoto wawili.
“Niliolewa nikiwa na umri wa miaka 15 nikazaa nikiwa na miaka 16, nikiwa na miaka 17 nikaongeza mtoto wa pili,” Amunga anasema.
Hadi kufikia kipindi hiki, Amunga alikuwa ameanza kuhisi afueni kidogo maishani mwake akilinganisha na maisha ambayo alipitia utotoni.
Chanzo cha picha, FLorence Amunga
‘Mtoto wangu mchanga ningemuacha kitandani angekuwa jivu’
Chanzo cha picha, FLorence Amunga
Baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya, hali ilibadilika ghafla makundi ya pande tofauti za kisiasa yalipoanza vurugu.
Wote walikuwa wanadai kushinda uchaguzi huo na hatimaye, ghasia zikaanza kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini Kenya.
Florence Amunga alikuwa akiishi katika eneo la Kibera ambalo ni miongoni mwa yalioathirika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Anasema siku ambayo nyumba yake ilichomwa moto, hali ilikuwa imeanza kubadilika.
“Mchana hakukuwa vizuri sana, vita vilikuwa vimeanza kutokea, mali ilikuwa inaporwa masokoni na biashara zimefungwa.
“Wakati tunaenda kulała, tulikuwa tunajiuliza kesho tutakula nini kwa sababu maduka na masoko yote yalikuwa yamefungwa na hatukuwa na chakula cha siku iliyofuata,” Amunga anasema.
“Wale waliokuwa na pesa walikuwa wameenda kwa marafiki na jamaa zao, lakini kwa wale ambao hawakuwa na pesa kama mimi walikuwa tu kwenye nyumba zao,” Amunga anaongeza.
Ilipofika nyakati za usiku, Florence alienda kulała kama kawaida na wanawe asijue kilichokuwa kinamsubiri. Usiku wa manane, nyumba yake ilichomwa moto akiwa ndani, amelala na watoto.
Kilichomuamsha ni moshi uliokuwa ukifuka na tayari ulikuwa umetanda kila sehemu huku wanawe wawili wakiwa bado kwenye usingizi mzito kitandani.
Amunga, kwanza alihisi kuchanganyikiwa, asijue anachokiona ni kweli au anaota. Lakini muda mfupi baadaye, aligundua moshi unaendelea kusongea alipokuwa na alipojaribu kutoka nje na wanawe akakumbana na changamoto nyingine ambayo kidogo ikimkatishe tamaa.
Mlango wake ulikuwa umefungwa kwa nje, hivyo hakuweza kufanya lolote.
“Sikuweza kutoroka kwa sababu nyumba haikuwa na dirisha. Waliwasha moto na kutufungia na nje.”
Kibaya zaidi, hata alipoamua kipiga mayowe hakuna aliyemsikia. Hali ilikuwa mbaya.
“Wakati napiga mayowe, mtoto mmoja alikuwa anachomeka, mwingine anachomeka na mimi pia ninachomeka,” Amunga anazungumza huku akilia.
Moto uliendelea kuwaka hadi ukawafikia na hapo ndipo alipompoteza mtoto wake akiwa anaona.
“Nilikuwa najaribu kumbeba huyu mdogo nimtoe kwenye kitanda, najaribu kumvuruta na huyu mwingine lakini nyumba yote imeshika moto. Nilimuweka yule mdogo chini akafia pale kwa sababu kitandani kulikuwa na chandarua na ikiwa ningemuwacha pale angekuwa jivu.”
Amunga anasema godoro lote na kitanda vilishika moto, sasa akawa yuko sehemu ya mlangoni na yule mtoto mkubwa.
Wakati walishakata tamaa ya kuishi, ndipo waliposikia majirani wamefika kuja kuwaokoa.
“Watu walikuja wakavunja mlango kwa nje lakini ukaniangukia nikiwa ndani,” Florence anasema.
Hili lilimfanya baadaye mwili wake ukawa umeegemea upande mmoja.
Majirani walichukua mabaki ya mtoto mchanga na akapelekwa chumba cha kuhifadhia maiti huku Florence na mtoto wake waliokolewa na kupelekwa katika hospitali iliyokuwa karibu kupata huduma ya kwanza.
Kwa bahati mbaya, walikuwa katika hali mbaya na wakaelekezwa moja kwa moja kwenda hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.
Amunga anasema alikuwa amechomeka vibaya sana kiasi kwamba hakuweza kumuona mtoto wake aliyesalia kwa sababu macho yake yalishindwa kufunguka.
Hakujua atokaye wala aingiae.
“Nilikuwa ninamwambia daktari anipeleke alikokuwa mtoto wangu ili nimpapase tu kwa sababu pia yeye alikuwa mdogo”.
Baada ya siku kadhaa, Florence anakumbuka siku ambayo hakumsikia mtoto wake akilia.
“Nilikaa siku nzima sikusikia mtoto wangu akilia, nikamuomba daktari aniambie ukweli, akaniambia mtoto wangu alikufa usiku wakati anawekwa damu na kupelekwa chumba cha kuhifadhi maiti,” Amunga anasema.
Baada ya kuambiwa ukweli, madaktari walianza kumfariji na kumuomba asilie sana.
“Nilimwambia daktari lazima nitalia, hao ni watoto wangu, tulikuwa watatu sasa nimebaki peke tangu, sijui nianzie wapi wala nimalizie wapi,” Amunga anasema huku akilia.
Hakika Florence Amunga akawa amesalia peke yake hospitalini, watoto wote wamekufa kwa mkasa wa moto wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi na yeye mwenyewe anapigania maisha yake.
Watoto hao walizikwa na wasamaria wema katika makuburi ya Lang’ata.
Wakati akiwa hospitalini, Amunga alikumbana na hali ngumu sana. Haikuwa rahisi kwake kukubali kilichotokea.
“Nilipitia kipindi kigumu sana kiasi kwamba wanasaikolojia walikuwa wanakuja kunipa ushauri nasaha kwa sababu nilikuwa ninalia mchana na usiku mzima,” Amunga anasema.
Kwa ushauri nasaha aliopokea kutoka kwa wataalam na wasamaria wema waliokuwa wanamtembelea na kumpa pole, alianza kupata nguvu taratibu ya kukubali kilichotokea.
Lakini amini usiamini, aliyekuwa mume wake hakuwahi kurejea tena. Amunga anafikiria pengine hilo lilichangiwa na gharama ya matibabu.
Safari ya uponaji
Safari ya uponaji ya Amunga pia haikuwa rahisi. Florence alifanyiwa apasuaji mara kumi.
“Nilikuwa nimelemaa upande mmoja, nikafanyiwa upasuaji mara 10, na kufanyishwa mazoezi ndio nikaanza kurejea vizuri,” Amunga anasema.
“Upasuaji haukuwa njia rahisi, madaktari walikuwa wananitoa ngozi sehemu zingine za mwili wanaziweka sehemu zilizoungua, inakuwa ni kama wananiweka kiraka.
“Mimi nilikuwa nimewekewa shuka kwa sababu kuanzia asubuhi hadi jioni, nilikuwa natoa maji. Ilibidi wanidunge sindano ili kusitisha maji yaliokuwa yanatoka,” Amunga anasema.
“Upande ambao ningelala, singeweza kuamka hadi mtu aje aniamshe”.
Amunga anasema alikuwa na uchungu mara tatu, kupoteza watoto wake, yeye kuchomeka kiasi cha kulemaa na mume wake kumuacha kipindi anamuhitaji zaidi.
Pia miongoni mwa yale ambayo Amunga bado anakumba hadi hii leo, hana masikio.
“Ukiniangalia masikio yangu, mimi sina masikio ndio maana najifunga kitambaa. Nilifungwa bendeji muda mrefu, masikio yangu yakaingia ndani,” Amunga anaonyesha jinsi masikio yake yalivyoingia ndani.
Anatumai kuwa ipo siku atapata mtu wa kumfadhili ili aweze kufanyiwa upasuaji na kuwekwa masikio bandia.
Hatimaye, Amunga alianza kukubali maisha yake jinsi yalivyo, akafanikiwa kupata mchumba mwingine na kuanza maisha yake upya.
Kwa bahati mbaya, mume wake alifariki wakati wa Covid-19 na kumuacha na watoto watatu ambão Florence anaendelea kulea.