Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, BBC Swahili
Klabu ya Grimsby Town imejikuta matatani licha ya ushindi wao mkubwa kwenye Kombe la Carabao wiki jana baada ya kutozwa faini ya pauni 20,000 kwa kumchezesha mchezaji aliyekuwa hajakamilisha usajili kwa wakati.
Katika mechi hiyo ya kusisimua, Grimsby waliibuka na ushindi dhidi ya Manchester United kwa njia ya mikwaju ya penalti, baada ya sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90.
Lakini furaha yao imeingia doa kufuatia makosa ya kiufundi wakati wa usajili.
Clarke Oduor ambaye ni raia wa Kenya, kiungo aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka Bradford City, alichezwa kama mchezaji wa akiba lakini baadaye ilibainika kuwa jina lake liliwasilishwa kwa EFL dakika moja na sekunde 59 baada ya muda wa mwisho wa saa 6:00 mchana (BST).
Clarke Oduor ndiye mchezaji pekee wa Grimsby kukosa penalti katika ushindi wao wa mikwaju 12-11 dhidi ya Manchester United.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka EFL, Grimsby ndio waliotoa taarifa kuhusu makosa hayo na walikuwa wazi kuwa hakuna udanganyifu wala nia ya kukiuka sheria.
“Klabu haikukusudia kuvunja sheria, na ilijiripoti yenyewe mara tu kosa lilipotambuliwa,” ilisomeka taarifa ya EFL.
Grimsby wametozwa pauni 10,000 taslimu , huku nyingine pauni 10,000 (jumla ya shilingi milioni 3.4) zikiwa zimeahirishwa hadi mwisho wa msimu endapo hakutakuwa na makosa mengine.
Manchester United wamesema hawana cha kusema kuhusu tukio hilo, huku wakipewa hadi Jumatatu ijayo kuwasilisha rufaa iwapo wataamua kupinga maamuzi ya EFL.
EFL ilisema kuwa hatua ya kutoa faini “ilizingatia kesi zilizotangulia” na ilifikiwa baada ya “uchambuzi wa kina wa ushahidi wote uliowasilishwa, pamoja na maamuzi ya awali katika mashindano ya kombe la Carabao.”
Kauli ya Grimsby Town
Vibonde hao ambao waliwavaa Manchester United katika raundi ya pili wanasema walimsajili Oduor dakika moja na sekunde 59 baada ya makataa ya usajili wa wachezaji kukamilika.
“Usajili wa mchezaji uliwasilishwa dakika moja baada ya muda wa mwisho, na kosa hilo halikutambuliwa mara moja kutokana na hitilafu ya kompyuta,” ilisomeka taarifa ya Grimsby.
“Tunapokea adhabu hii kwa uelewa, na tunatambua umuhimu wa kufuata sheria za mashindano. Kosa hili halikuwa la makusudi, na klabu ilijitokeza yenyewe kutoa taarifa pindi lilipogundulika.”
“Tumechunguza upya taratibu zetu na kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kosa kama hili halijirudii.”
“Tunashukuru bodi ya EFL kwa kutambua ushirikiano wetu na nia njema tuliyoonyesha.”
Safari ya michezo ya Clarke Sydney Omondi Oduor
Mzaliwa huyo wa Nairobi ambaye anaweza cheza kama kiungo wa kati na pia beki wa kushoto amefanikiwa kupanda viwango katika soka ya Uingereza.
Alianza katika akademia ya Leeds United, alikopata nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2019 kabla ya kujiunga na Barnsley ambapo alifunga bao maarufu la dakika za mwisho kuwasaidia kusalia katika ligi ya daraja la pili mwaka 2020.
Baada ya kuichezea Hartlepool kwa mkopo kisha akapata mkataba wa kudumu Bradford City, Hatua yake ya kujiunga na Grimsby ilitarajiwa kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara. Hata hivyo, faini hiyo imetia doa ujio wake.
katika jukwaa la kimataifa, Oduor ameiwakilisha timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars, mechi yake ya kwanza ilikuwa ushindi wa 2–1 dhidi ya Zambia mwezi Oktoba mwaka 2020. Uwezo wake wa kucheza katika nafasi zaidi ya moja umempa nafasi nzuri ya kujumuishwa kwenye kikosi cha Kenya.
Licha ya faini hiyo, Ushindi wa Grimsby dhidi ya Manchester United kupitia mikwaju ya penalti bado unasalia, na Oduor anatarajiwa kutumika sana kwenye kikosi cha timu hiyo katika mechi za ligi ya daraja la nne nchini uingereza.
Grimsby 2-2 Man Utd (12-11 kwa mikwaju ya penalti, Kombe la Ligi, 2025)
Matokeo haya yalishangaza si tu kwa jinsi yalivyotokea bali pia kwa ukubwa wake.
Grimsby Town, timu ya Ligi ya Pili, iliishinda Manchester United kutoka Ligi Kuu.
Sio kwamba walishinda tu, Grimsby walitoka kifua mbele, wakifunga mabao mawili ya haraka kupitia Charles Vernam na Tyrell Warren ndani ya dakika 30 za kwanza.
Bryan Mbeumo akarejesha matumaini kwa United kabla ya Harry Maguire kusawazisha dakika ya 89.
Penalti zikafuata, ikageuka pambano la kusisimua, kila mchezaji wa pande zote akapiga. Oduor (Grimsby) na Cunha (Man Utd) ndio pekee walikosa kati ya wachezaji 11 wa kila upande waliopiga.
Wachezaji walirudia tena penalti na baada ya Darragh Burns kufunga penalti ya 12-11, Mbeumo aligonga mwamba na Grimsby wakashinda.
Si Mara ya Kwanza
Hili si tukio la kwanza klabu kuingia matatani kwa kumtumia mchezaji ambaye hajasajiliwa kikamilifu katika Kombe la Carabao.
Mnamo 2019 Liverpoolal walimchezesha Pedro Chirivella bila kibali cha FIFA na wakatozwa pauni 200,000 (nusu ikiwa ya kuahirishwa).
Nao Accrington Stanley mwaka 2016 walimuingiza uwanjani Janoi Donacien akiwa hajakamilisha usajili na wakapigwa faini ya pauni 5,000 ya kusubiri.
Sunderland nao hawakuponea faini mnamo mwaka 2013 walimtumia Ji Dong-won bila ruhusa, wakaadhibiwa kwa pauni 25,000 na pia wakafungiwa kwenye mechi kadhaa. Ni mechi walioicharaza MK Dons.
Licha ya sakata hii, Kikosi cha David Artell sasa kinaelekeza macho yake kwenye raundi ya tatu ya Carabao Cup ambapo kitaumana na klabu ya Championship Sheffield Wednesdayinayopambana kutoshuka daraja.