Chanzo cha picha, HP
-
- Author, Na Yusuph Mazimu
- Nafasi,
Ripoti mpya ya Africa Wealth Report 2025, iliyotolewa na kampuni ya ushauri wa uwekezaji wa kimataifa Henley & Partners kwa kushirikiana na New World Wealth, inaonyesha sura mpya ya bara la Afrika katika ramani ya utajiri duniani.
Tanzania imeendelea kufanya vyema kwa nchi za Afrika Mashariki. Ikiwa ni nchi pekee katika orodha ya nchi saba zenye ma bilionea barani Afrika.
Kwa sasa, Afrika ina jumla ya mabilionea 25, centi-milionea 348 (wale wenye utajiri wa angalau dola milioni 100), na zaidi ya mamilionea 122,500.
Hali hii inaonyesha mabadiliko makubwa kutoka miaka ya mwishoni mwa karne ya 20, wakati ambapo kulikuwa na mabilionea wachache sana huku uchumi wa mataifa mengi ya Afrika ukiwa umedorora.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi zinazongoza kwa idadi ya mabilionea barani Afrika ni:
- Afrika Kusini – ina mabilionea 8
- Misri – mabilionea 7
- Morocco – mabilionea 4
- Nigeria – 3 mabilionea 3
- Algeria -1 bilionea 1
- Seychelles -bilionea 1
- Tanzania – bilionea 1
Kwa pamoja, mataifa haya saba yana karibu asilimia 88 ya mabilionea wote wa Afrika. Nchi ya Tanzania si haba imeingia kama nchi pekee kutoka Afrika Mashariki kuwa na angalau bilione mmoja.
Kenya haina bilionea hata mmoja kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu, ila ina idadi kubwa ya mamilionea kuliko Tanzania na nchi zingine Afrika Mashariki.
Kenya imeingia tano bora barani Afrika kwa nchi zenye mamilionea wengi zaidi, ikiwa na mamilionea wapatao 6,800.
Afrika Kusini kinara wa utajiri Afrika
Chanzo cha picha, Joberg
Ripoti hiyo inaitaja Afrika Kusini kama kitovu kikuu cha utajiri barani Afrika ikiongeza kwa kuwa na milionea 41,100, kiwango kikubwa zaidi sawa na jumla ya mamilionea wote wa nchi tano zinazofuata: Misri, Morocco, Nigeria, na Kenya.
Misri inashikilia nafasi ya pili kwa kuwa na milionea 14,800, ikifuatiwa na Morocco (7,500), Nigeria (7,200) na Kenya (6,800).
Ripoti inabainisha kuwa idadi ya mamilionea barani Afrika inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 65 ndani ya muongo mmoja ujao, ikiashiria fursa kubwa kwa uwekezaji wa muda mrefu.
Hii inakuja huku uchumi wa nchini za kusini mwa Jangwa la Sahara ukitabiriwa kukua kwa 3.7% mwaka 2025, na kufikia 4.1% mwaka 2026, viwango vinavyowazidi Ulaya (0.7%) na Marekani (1.4%).
Nchi zinazokua na zinazodorora
Mauritius imeongoza bara Afrika kwa ukuaji wa watu wenye utajiri mkubwa na wa hali ya juu, high-net-worth individuals (HNWI) kwa asilimia 63 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ikichochewa na uthabiti wa kisiasa na sera za kodi rafiki.
Rwanda (+48%) na Morocco (+40%) pia zimepiga hatua kubwa.
Hata hivyo, baadhi ya nchi zimeona kuporomoka kwa idadi ya mamilionea, ikiwemo Nigeria (-47%), Angola (-36%) na Algeria (-23%).
Kwa mujibu wa Dominic Volek, kiongozi wa Idara ya wateja binafsi wa Henley & Partners, Afrika sasa imejitokeza kama mhimili muhimu wa utajiri duniani.
“Sekta ya uhamiaji wa uwekezaji sasa inafanya kazi pande zote mbili: Waafrika wanatafuta fursa zaidi za kimataifa, huku wawekezaji wa nje wakitazama Afrika kama eneo la uwekezaji wa muda mrefu na thabiti,” anasema.