Chanzo cha picha, Geena Truman
Jengo la Ziggurat katika mji wa Uru, Iraq ni kazi ya kuvutia ya uhandisi ambayo imehifadhiwa vizuri katika jiji muhimu la kale.
Miaka 4,000 iliyopita, sehemu hii ya jangwa huko Iraq ilikuwa kitovu cha ustaarabu. Leo, magofu ya jiji la Uru, ambalo hapo awali lilikuwa kitovu cha utawala wa Mesopotamia, yako katikati ya jangwa lisilo na watu.
Ili kufika hapa, nilipanda teksi iliyokuwa ikipanda na kushuka jangwani kwa saa nyingi hadi hatimaye nikaona jengo maarufu la jiji hilo: Ziggurat, hekalu kubwa la umri wa miaka 4,100 lenye ngazi kubwa.
Majengo ya kwanza ya Ziggurati yana umri mrefu zaidi ya piramidi za Wamisri, kuna mabaki ya majengo hayo huko Iraq na Iran.
Majengo haya ya kupendeza yana kazi za kidini, lakini hutofautiana kwa njia fulani na piramidi. Ziggurati hazina vyumba ndani, lakini kuna makaburi ndani, na juu kuna mahekalu.
Madeline Romer, mtaalam wa Mashariki ya Kati ya kale katika Chuo Kikuu cha Case Western Reserve nchini Marekani anasema, “mahekalu ya mwanzo yalikuwa ni miundo ya chumba kimoja. Baada ya muda, mahekalu yalijengwa upya na kupanuliwa mara kwa mara, yakiongezeka ukubwa.”
Jengo la Ziggurat la Uru lilijengwa kama miaka 680 baada ya piramidi za kwanza. Kulingana na Romer, Mesopotamia ilikuwa mahali pa kwanza kuzaliwa umwagiliaji: watu wa Uru walichimba mifereji ya kudhibiti mtiririko wa maji na kumwagilia mashamba kupitia kingo za Mto Euphrates.
Kuibuka na kupotea
Chanzo cha picha, Truman
Uru pia inaaminika ndipo sehemu alipozaliwa Nabii Ibrahim.
“Katika Mesopotamia, kila jiji lilianzishwa na kujengwa kama makao ya mungu au mungu wa kike … ambaye alikuwa na jukumu kama mlezi wa jiji na mamlaka ya kisiasa,” anasema Romer.
Huko Uru, kulikuwa na Mungu Nana, mungu wa mwezi. Jengo hilo la ziggurati lilijengwa kama makao ya kidunia na hekalu la Mungu huyo.
Eneo la chini la hekalu bado lipo, ingawa hekalu limetoweka. Wataalamu wametumia teknolojia mbalimbali na maandishi ya kale (kutoka kwa wanahistoria kama vile Herodotus na Agano la Kale la Biblia) ili kuelewa jengo hili.
“Majengo ya Ziggurates yaliundwa kwa muundo wa piramidi yenye sehemu ya juu bapa na sehemu ya ndani iliyotengenezwa kwa udongo uliochomwa na jua….”, ameandika Amelia Sparavigna, mtaalam wa picha za kiakiolojia katika Chuo Kikuu cha Polytechnic cha Turin, katika makala yake ya 2006 na “A Monggurat”.
Kulingana na mabaki yaliyopatikana katika eneo hilo, inaaminika kwamba Ziggurat ya Uru lilikuwa ni hekalu la rangi ya bluu. Msingi wake pekee una matofali zaidi ya 720,000 ambayo yamewekwa kwa uangalifu juu ya kila mmoja, kila moja likiwa na uzito wa kilo 15.
Licha ya mafanikio hayo yote, kufikia karne ya sita BK, jiji hili kuu lililokuwa limestawi lilikauka. Mto Eufrati ulibadilika, na jiji hilo halikuwa tena na maji, na hivyo kulifanya lisiwe na watu. Uru na ziggurati yake iliachwa, hatimaye kuzikwa chini ya mlima wa mchanga uliowekwa na upepo na wakati.
Ilichukua hadi mwaka 1850 kwa ziggurat kugunduliwa tena; baadaye katika miaka ya 1920, mwanaakiolojia Mwingereza Sir Leonard Woolley alichimbua eneo hilo, akifichua kile kilichobaki, na kukuta magamba ya dhahabu, sanamu za kuchonga, vinubi, na makaburi.
Wakati wa Saddam
Chanzo cha picha, GETTY
Wakati wa Vita vya Ghuba vya 1991, Saddam Hussein aliegesha ndege zake mbili za kivita za MiG karibu na jengo hilo, akitumaini kwamba hilo lingezuia mashambulizi ya Marekani na nchi za kigeni. Kwa bahati mbaya, jengo la ziggurat liliharibiwa kidogo.
Mwaka 2021, Iraqi ilifungua milango yake kwa nchi mbali mbali za Magharibi, na utalii uliongezeka polepole. Janet Newenham, mwandishi wa habari wa Ireland, alitembelea Iraq muda mfupi baada ya utalii kufunguliwa.
Tangu wakati huo, amefanya ziara kadhaa za vikundi kwenye eneo hilo. “Katika safari yetu ya kwanza Julai 2021, hatukuona mtalii mwingine hata mmoja. Hadi safari yangu Aprili 2022, ndipo tuliona vikundi vidogo vya watalii…wanne au watano pamoja kwa wakati mmoja”