Chanzo cha picha, Netflix
-
- Author, Darío Brooks
- Nafasi, BBC News Mundo
Katika mji wa mpakani wa Tijuana, Mexico, kuna kikosi maalum kinachofanya kazi kwa ufanisi mkubwa: International Liaison Unit (ILU), maarufu kama “Gringo Hunters”.
Kikosi hiki kilichokuwa kikiongozwa na Abigail Esparza Reyes, hufuatilia na kuwakamata wahalifu wa Marekani waliotoroka haki na kujificha nchini Mexico.
Mnamo Aprili tarehe 9 mwaka 2025, ILU ilimteka César Hernández, aliyekimbia kifungo cha mauaji huko California alipokuwa akihamishwa jela mnamo 2024 mwezi Disemba.
Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 35 alitorokea Tijuana ambapo alikuwa akijaribu kuanzisha maisha mapya.
ILU, ambayo inafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na mashirika ya shirikisho ya Marekani inayoomba kukamatwa huko Mexico, ilikuwa imempata Hernández. Mnamo saa 14:00, operesheni ya kumkamata ilianza.
“Walikuwa katika eneo la makazi ya kibinafsi. Walikuwa wakifuatilia viingilio na kutoka,” anaelezea Eduardo Villa Lugo, mwandishi wa habari za usalama kutoka jimbo la Baja California.
Lakini wakati wa operesheni hiyo mambo yalienda sengemnenge.
”Walipokuwa wakiingia, Abigail akiongoza kikosi hicho, walimiminiwa risasi. Ikawa mchezo wa paka na panya huku Polisi nao wakijibu kwa kuwafyatulia risasi. Hata hivyo washukiwa walitoroka kupitia mlango wa nyuma wa nyumba,” anaeleza mwanahabari huyo.
Risasi iliyofyatuliwa kutoka ghorofa ya pili ilimpata na kumuumiza Abigail Esparza. Ingawa usaidizi wa matibabu ulipatikana kwa haraka alifariki dunia muda mfupi baadaye akiwa hospitalini.
Hernández alitoroka akiwa uchi, juu ya paa, hadi alipopata nguo kwenye gari lililokuwa limeegeshwa.
Chanzo cha picha, SSC
Siku chache baadaye, Cesar alikamatwa katika eneo lingine huko Tijuana. Lakini tayari hasara ilikuwa ishatokea.
kifo cha shujaa, kilichoacha pengo katika historia ya ILU.
Kwa zaidi ya miaka 20, kikosi hiki kimewakamata zaidi ya wahalifu 1,500, karibu wote kutoka Marekani wanaojificha katika eneo la mpakani wa Baja California.
Ufanisi wao unatokana na uchambuzi wa taarifa za kijasusi pamoja na mipango ya kina inayotekelezwa kwa uangalifu jambo lililotambulika na mamlaka za Mexico na Marekani.
Kwa vyombo vya habari, kazi yao imevutia umakini mkubwa.
Mnamo 2022, gazeti la Marekani The Washington Post lilichapisha ripoti ya kina juu ya maafisa hao, likiwaita “gringo hunters.”
Jina hilo halikuanzishwa rasmi na idara, bali likachukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari na baadaye Netflix kwa kipindi chake kinachoonyesha operesheni ya ILU.
Idara ya ILU hufanya kazi kwa karibu na mashirika ya Marekani kama FBI, DEA, na wakuu wa idara ya polisi Marekan, jambo linaloifanya kuwa ya kipekee miongoni mwa vikosi vya usalama vya Mexico ambavyo huonekana kuwa havina uaminifu wa kutosha.
Mafanikio yao yamechangiwa na matumizi ya ujasusi wa hali ya juu, mafunzo kutoka Marekani, na mbinu za kimyakimya za kioperesheni.
”Kamanda Abigail alikuwa nguzo ya tabia ya kipekee na kujitolea kuhudumia jamii yake. Atakumbukwa kwa ujasiri, utumishi, na dhabihu yake kuu,” ilisema Ofisi ya Sherifu wa San Diego, upande mwingine wa mpaka.
Baada ya kifo hicho, ILU ilijiondoa katika vyombo vya habari.
BBC Mundo ilitaka kufanya mahojiano na idara hiyo, lakini haikupokea majibu mazuri.
Chanzo cha picha, Getty Images
Villa Lugo anasema kwamba baada ya kifo hicho, U.S. Marshals walishiriki katika tukio la kumpa familia yake msaada, na Mexico ilifanya heshima rasmi huku Marekani pia ikihudhuria.
Mchambuzi wa masuala ya usalama Victor Sánchez anaeleza kwamba: “Faida kuu ya ILU ni kwamba walipewa majukumu, yakawa na mafanikio, na hivyo kujenga uhusiano wa kuaminiana” na mamlaka za Marekani.
“Mara nyingi kuna kusita kwa baadhi ya mamlaka za Marekani kushiriki habari na mamlaka za Mexico kutokana na kiwango cha rushwa na udhaifu wa kitaasisi,” anafafanua.
Rapid capture and handover
Hakuna idara nyingine ya usalama katika kiwango cha kitaifa au majimbo nchini Mexico inayofanana na kikosi cha ILU cha Baja California.
Msemaji wa Wizara ya Usalama na Ulinzi wa Raia alieleza kuwa, ingawa hushirikiana na Marekani kuwakamata wahalifu wa kimataifa, hakuna kikosi kingine kilicho bobea kwa wahalifu wa kigeni, ikiwemo mmoja wa wahalifu 10 wanaosakwa na FBI mwezi Machi.
Katika Baja California, kwa upande mwingine, wengi wa mawakala wake na viongozi wa timu wamefunzwa ujasusi na mipango ya kivita nchini Marekani.
“Baadhi ya waratibu hata wana mafunzo ya kijeshi au nusu ya kijeshi katika operesheni na kubuni mkakati,” Villa Lugo anabainisha.
Mamlaka za Marekani zinapogundua kuwa mtu anayetafutwa amevuka mpaka na kuingia Mexico, wanaweza kuomba usaidizi wa timu kama vile ILU ili kumpata na kumkamata, na humkabidhi kwa mamlaka za Marekani mara moja badala ya kuwaweka chini ya sheria za uhamiaji wa Mexico.
“Sehemu ya mchakato wa uchunguzi hufanyika Marekani. Wanasema, ‘Tumepata akaunti ya benki, au ishara simu ya mkononi inatumika, au barua pepe kutoka kwa anwani ya IP iliyo na eneo fulani,’ na kwa kuwa hawana mamlaka yoyote nchini.
Wakala wa kitaalam huandaa mpango wa ufuatiliaji na, mahala mlengwa yupo, huandaa na kutekeleza operesheni ya kukamata.
Kwa sababu walengwa ni watu binafsi, hii inahitaji idadi ndogo ya mawakala, tofauti na shughuli kubwa za kupambana na dawa za kulevya za mamlaka nyingine za serikali au kitaifa.
Chanzo cha picha, Getty Images
Hii pia inawaruhusu kufanya kazi kwa busara zaidi na kimya kimya.
Wanaweza kutumia magari na nguo bila nembo ya wakala wa usalama wa serikali wakati wa kufanya ufuatiliaji na ujasusu, ili wasiwatahadharishe walengwa.
Wanapoanzisha operesheni, wanachukua hatua haraka: wanazingira walengwa wao na kuwakamata, wakijitambulisha kuwa maajenti wa usalama. Na kama vile kukamatwa kwao kulivyo haraka, ndivyo kukabidhiwa kwao kwa mamlaka za Marekani.
“Hawatawakamata na kuwafikisha mbele ya mahakama ya Mexico ili wakabiliane na kesi za kuwafukuza nchini. Inachukuliwa kuwa mtu huyo aliingia kama mtalii, kwamba wamekaa muda zaidi kuliko walivyoruhusiwa (miezi mitatu), na kwa hiyo, wanarudishwa nchini mwao,” anaelezea Sánchez.
Wafungwa hao hupelekwa kwenye vivuko vya mpaka wa Marekani na kuachiliwa mbele ya maajenti wa Marekani, ambao huwaweka chini ya ulinzi mara moja na kuwapeleka popote wanapotafutwa.
Wanahisi ‘huru’ wakiwa Mexico
Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya wageni nchini Mexico imeongezeka, lakini idadi ya raia wa Marekani imeongezeka, kwa sasa wanakaribia karibu milioni mbili.
Wamexico wengi huwa na urafiki kwa wageni, ambayo hufanya nchi kuwa mahali salama kwa wale wanaokimbia haki nchini Marekani au nchi nyingine.
“Ni jambo la kawaida sana kwa watu kukimbilia Mexico kwa sababu tatu: moja ni udhaifu mkubwa wa kitaasisi, na mifumo michache ya uchunguzi; pili, kitamaduni, kuna taswira chanya ya wageni – wanaelekea kupokelewa vyema kwa vile ni nchi ya kitalii, na hakuna shaka ikiwa wale wanaokuja wamefanya uhalifu; na tatu, kutokana na kiwango cha kipato, watu wasio na pesa nyingi wanaweza kuamini kuwa wana pesa.” hivyo ndivyo Sanchez anaamini.
Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini mienendo ya kijamii ya mpaka pia ni tofauti na Mexico au Marekani.
Mpaka wa kaskazini-magharibi, haswa, ni moja wapo ya mpaka ulio na shughuli nyingi zaidi ulimwenguni.
“Maisha ya kitamaduni ya eneo hilo yameyeyuka na kuiga zaidi mtindo wa maisha wa ulimwengu. Tijuana ina uhusiano mkubwa na San Diego katika suala la kazi, uchumi, na kila kitu. Na watu wengi wanaoishi San Diego wana jamaa huko Tijuana. Ikiwa mtu atafanya uhalifu huko [huko California], huvuka na kujificha katika Tijuana, ambayo ni jiji kubwa sana,” anaelezea Villa Lugo.
Chanzo cha picha, Netflix
Uhalifu unaoonekana katika kesi zinazofuatiliwa na ILU kwa kawaida ni za jinai: mauaji, ubakaji, vurugu, au kutoroka jela, lakini kwa ujumla huwahusisha watu ambao si sehemu ya shirika kubwa la uhalifu au walanguzi wa dawa za kulevya.
“Kama genge la ulanguzi wa dawa za kulevya au genge la wizi wa mafuta litahusika, inawezekana kwamba genge hilo limejipenyeza kwa polisi na hakutakuwa na ushirikiano na Marekani,” Sánchez anaonyesha.
Na kwa kuwa uhalifu wa ulanguzi wa dawa za kulevya nchini Mexico hushitakiwa na mamlaka ya serikali pekee, mamlaka za mitaa zina uwezo mdogo wa kuchukua hatua hata dhidi ya washukiwa wanaojulikana kuhusika katika uhalifu huu.
“Walengwa wengi wa ulanguzi wa dawa za kulevya hawana hata hati ya kukamatwa na mamlaka za ndani. Tunatania kwamba kama wangetaka, watu hawa wangeweza kupata leseni ya udereva kwa urahisi kwa sababu hawatakiwi huko Baja California,” anasema Villa Lugo.