
Vita vilivyoanza kati ya Israel, Hamas, na makundi mengine ya Wapalestina yenye silaha katika Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, ni sehemu moja tu ya mfululizo unaoendelea wa makabiliano, ghasia, mauaji, na mashambulizi ya kujitoa mhanga tangu kuanzishwa kwa Harakati ya Upinzani ya Kiislamu, inayojulikana kama Hamas, mnamo 1987 na marehemu Mpalestina, Ahmed Yassin.
Vuguvugu hilo lilianzisha makumi ya mashambulizi ya kujitoa muhanga ndani ya Israel, na kuua mamia ya Waisraeli, wakati wa Intifada ya Kwanza, iliyoanza katika Ukanda wa Gaza mwaka 1987 ilipokuwa chini ya utawala wa Israel. Ilienea hadi Ukingo wa Magharibi na kumalizika kwa kusainiwa kwa Makubaliano ya Oslo mnamo 1993.
Intifadha ya Pili, ambayo ilizuka baada ya kiongozi wa upinzani wa wakati huo wa Israel, Ariel Sharon kuingia Msikiti wa Al-Aqsa mwaka 2000, ilikuwa na umwagaji damu na vurugu zaidi kuliko Intifadha ya Kwanza, ambapo watu 4,200 waliuawa kwa pande zote mbili, kiwango cha Muisraeli mmoja kuuawa kwa kila Wapalestina watatu.
Israel imefanya mauaji kadhaa yakiwalenga viongozi wa kundi la Wapalestina, shambulizi la hivi punde zaidi likiwa ni shambulio la anga kwenye mji mkuu wa Qatar, Doha, Septemba 9. Israel ilijaribu kuwauwa viongozi wa Hamas huko Doha, lakini Hamas ilitangaza kuwa jaribio hilo “lilishindwa.”
Ripoti zimesambaza majina kadhaa mashuhuri katika orodha inayolengwa, akiwemo mkuu wa harakati hizo katika Ukanda wa Gaza, Khalil al-Hayya, pamoja na mkuu wa zamani wa ofisi ya kisiasa, Khaled Meshaal.
Ifuatayo ni orodha ya viongozi mashuhuri wa Hamas ambao waliuawa, au kunusurika katika jaribio la kuuawa na Israel hadi mwaka 2025:
Khalil Al-Hayya
Chanzo cha picha, Getty Images
Khalil Ismail Ibrahim Al-Hayya ni mmoja wa watu mashuhuri Hamas ilithibitisha kunusurika katika jaribio la mauaji lililotekelezwa na Israel huko Qatar mnamo Septemba 9, 2025.
Al-Hayya, anayeitwa “Abu Osama,” ni mmoja wa viongozi mashuhuri wa kisiasa wa Hamas na mjumbe wa Ofisi yake ya Kisiasa. Alizaliwa katika Ukanda wa Gaza mnamo Januari 1960, Al-Hayya alipata shahada ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza mnamo 1983, shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Jordan mnamo 1989, na Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kurani Tukufu na Sayansi ya Kiislamu nchini Sudan mnamo 1997, zote zikiwa na utaalamu unaohusiana na sheria za Kiislamu.
Amekuwa akijihusisha na siasa tangu kuanzishwa kwa Hamas, na alishiriki katika Intifadha ya Kwanza mwaka 1987. Aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Palestina baada ya kushinda uchaguzi wa 2006, na alikuwa mkuu wa kambi ya Hamas humo.
Alikaa miaka mitatu katika magereza ya Israel katika miaka ya 1990 kwa tuhuma za ugaidi.
Aliongoza duru kadhaa za mazungumzo ya kusitisha mapigano na Israel. Inasemekana alinusurika majaribio mawili ya mauaji na kupoteza wanafamilia kadhaa kutokana na mashambulizi ya Israel.
Alijulikana kwa uhusiano wake wa karibu na Iran, utawala wa Assad huko Syria, na Hezbollah, na alishiriki katika kuimarisha uhusiano wa harakati na vyama hivi.
Hivi sasa anachukuliwa kuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa Hamas, haswa baada ya vifo au kutoweka kwa viongozi kadhaa wa Hamas wakati wa vita vinavyoendelea.
Al-Hayya anaongoza ujumbe wa harakati hiyo unaojadili maendeleo ya hivi karibuni kuhusiana na vita katika Ukanda wa Gaza, na pia anaongoza harakati katika Ukanda wa Gaza.
Khaled Meshaal
Chanzo cha picha, AFP
Khaled Meshaal, mkuu wa zamani wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, pia anaripotiwa kuwa mmoja wa watu mashuhuri walionusurika katika jaribio la mauaji ya Israel katika shambulio la Doha.
Khaled Meshaal, ambaye alizaliwa katika Ukingo wa Magharibi mwaka 1956, anachukuliwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa Hamas.
Chini ya maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, shirika la kijasusi la Israel la Mossad lilijaribu kumuua Meshaal mwaka 1997 alipokuwa akiishi Jordan.
Maafisa wa Mossad waliingia Jordan wakiwa na pasipoti ghushi za Canada na Meshaal alidungwa sindano yenye sumu wakati akitembea kando ya barabara.
Mamlaka ya Jordan iligundua jaribio la mauaji na kuwakamata maafisa wawili wa Mossad.
Marehemu Mfalme Hussein wa Jordan alimwomba waziri mkuu wa Israeli dawa ya ya kumtibu Meshaal kuzuia kifo chake kutokana na sumu aliyodungwa. Akikabiliwa na shinikizo kutoka kwa Rais wa wakati huo wa Marekani Bill Clinton, Bw Netanyahu alitoa dawa baada ya awali kukataa ombi hilo.
Meshaal, ambaye anaishi Qatar, alitembelea Ukanda wa Gaza kwa mara ya kwanza mwaka 2012. Alipokelewa na maafisa wa Palestina na umati wa Wapalestina ulijitokeza kumkaribisha.
Hamas ilimchagua Ismail Haniyeh kumrithi Meshaal kama mkuu wa ofisi yake ya kisiasa mwaka 2017, na Meshaal akawa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya kundi hilo nje ya nchi.
Yahya Sinwar
Chanzo cha picha, Getty Images
Yahya Sinwar ni kiongozi wa Hamas ndani ya Ukanda wa Gaza. Israel inaamini kuwa ndiye aliyepanga shambulio hilo ambalo halijawahi kutokea tarehe 7 Oktoba 2023.
Sinwar alizaliwa katika kambi ya wakimbizi ya Khan Younis huko Gaza mnamo 1962.
Mwaka mmoja baada ya Hamas kuanzishwa mwaka 1987, aliunda huduma yake ya usalama wa ndani, ambayo miongoni mwa mambo mengine ililenga wanaodaiwa kuwa ni Wapalestina wanaoshirikiana na Israel.
Sinwar alikamatwa na Israeli mara tatu. Alihukumiwa vifungo vinne vya maisha mwaka 1988 kwa kupanga utekaji nyara na mauaji ya wanajeshi wawili wa Israel na mauaji ya Wapalestina wanne.
Hata hivyo, mwaka 2011 alikuwa miongoni mwa wafungwa 1,027 wa Wapalestina na Waisraeli wa Kiarabu walioachiliwa na Israel kwa kubadilishana na mwanajeshi wa Israel aliyetekwa na Hamas kwa zaidi ya miaka mitano.
Sinwar alirejea katika nafasi yake ya kiongozi mashuhuri katika Hamas na aliteuliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya kundi hilo katika Ukanda wa Gaza mwaka 2017, na kumfanya kuwa kiongozi wa Hamas katika eneo hilo.
Mnamo 2015, Marekani ilijumuisha jina la Sinwar kwenye orodha yake ya “magaidi wa kimataifa”.
Israel wiki jana ilitangaza kumuua Sinwar na kutoa video iliyoonesha dakika zake za mwisho kabla ya mauti kumkumba.
Ismail Haniyeh
Chanzo cha picha, Reuters
Aliuawa, katika shambulio la angani, kwenye jengo alilokuwa akiishi wakati wa ziara yake mjini Tehran tarehe 31 Julai, 2024. Iran na Hamas zimeilaumu Israel kwa shambulio hilo.
Mwanachama mashuhuri wa Hamas mwishoni mwa miaka ya 1980, Israel ilimfunga Haniyeh kwa miaka mitatu mwaka 1989 huku ikikabiliana na uasi wa kwanza wa Wapalestina.
Kisha alihamishwa mwaka 1992 hadi ardhi isiyomilikiwa na nchi yoyote kati ya Israel na Lebanon, pamoja na baadhi ya viongozi wa Hamas.
Baada ya mwaka mmoja alirudi Gaza. Mnamo 1997 aliteuliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kiongozi wa kidini wa Hamas, akiimarisha nafasi yake.
Haniyeh aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Palestina mwaka 2006 na Rais Mahmoud Abbas baada ya Hamas kushinda viti vingi zaidi katika uchaguzi za kitaifa. Lakini alifukuzwa kazi mwaka mmoja baadaye huku kukiwa na ghasia mbaya huko Gaza, na Hamas hatimaye kukiondoa chama cha Fatah cha Bw Abbas kutoka Ukanda wa Gaza.
Haniyeh alipinga kufukuzwa kwake kama “kinyume cha katiba”, na Hamas iliendelea kutawala huko Gaza.
Alichaguliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa yenye nguvu zaidi ya Hamas mnamo 2017, na kumfanya kuwa kiongozi wa jumla.
Mnamo mwaka wa 2018, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilimtaja Haniyeh kuwa gaidi. Alikuwa ameishi Qatar kwa miaka kadhaa iliyopita.
Mohammed Deif
Chanzo cha picha, Reuters
Mohammed Deif alikuwa mkuu wa Brigedi ya Izz al-Din al-Qassam, kitengo cha kijeshi cha harakati ya Hamas. Alikuwa mtu anayesakwa sana na Israeli kwa miongo kadhaa, na aliuawa katika shambulio la anga la Israeli mwezi uliopita, Israeli inasema. Hamas haijathibitisha hili.
Deif, mtu ambaye ni vigumu kujua aliko na shughuli zake, alijulikana kwa Wapalestina kama The Mastermind, na kwa Waisraeli kama Paka mwenye Maisha Tisa.
Mamlaka ya Israeli ilimfunga gerezani mwaka wa 1989 wakati wa intifada ya kwanza ya Wapalestina (maasi), na kumwachilia baada ya mwaka mmoja na nusu. Muda mfupi baadaye aliunda Brigedi ya al-Qassam, kwa lengo la kuwakamata wanajeshi wa Israel.
Pia alisaidia katika ujenzi wa mahandaki yaliyowawezesha wapiganaji wa Hamas kuingia ndani ya Israel kutoka Gaza.
Deif alishutumiwa na Israel kwa kupanga na kusimamia mashambulizi ya mabasi yaliyoua makumi ya Waisraeli mwaka 1996, na kuhusika katika kuwakamata na kuwaua wanajeshi watatu wa Israel katikati ya miaka ya 1990. Alikamatwa na Mamlaka ya Palestina mwaka 2000, lakini alitoroka miezi saba baadaye mwanzoni mwa intifadha ya pili.
Alikuwa mtu anayetafutwa sana na Israeli, lakini tangu wakati huo hakuna aliyejua aliko.
Majaribio makubwa zaidi ya kumuua yalikuwa mwaka wa 2002: Deif alinusurika lakini alipoteza jicho lake moja. Israel inasema pia alipoteza mguu na mkono, na tatizo la kuongea.
Israel ilijaribu na kushindwa tena kumuua Deif wakati wa shambulio la 2014 kwenye Ukanda wa Gaza, lakini ikaua mke wake na watoto wake wawili.
Deif alikuwa mmoja wa watu walioshutumiwa kupanga shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, 2023. Israel ilisema ilimuua katika shambulio la anga kwenye boma katika eneo la Khan Younis huko Gaza tarehe 13 Julai.