Watu wawili wamefariki na wengine 6 wamejeruhiwa hapo jana baada ya gari la matangazo la mashindano ya baiskeli ya Tour du Rwanda kupoteza njia na kuwagonga watazamaji, waandaji wa mashindano hayo makubwa zaidi barani Afrika wamethibitisha.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji kupitia ukurasa wa X, imesema tukio hilo lilitokea wakati wa mzunguko wa kwanza mashariki mwa mji wa Gabiro.
“Gari ya matangazo ilipoteza njia na kuwagonga watazamaji kadhaa”, taarifa ilisema ambapo ikaongeza kuwa “kwa huzuni watu wawili walipoteza maisha na wengine 6 walijeruhiwa”.
Polisi ya Rwanda tayari imeanzisha uchunguzi kubaini kilichosababisha ajali hiyo, waandaji wakisema watu waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu, huku wakitoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao.
Hatua ya kwanza ya mashindano haya, ilifanyika huku mvua kubwa ikinyesha katika maeneo mengi ya nchi, mwendesha baiskeli rai awa Israel, Itamar Eihorn akishinda mzunguko wa kwanza.
Mwezi Septemba mwaka uliopita, Rwanda ilikuwa mwenyeji wa mashindano ya kwanza makubwa ya baiskeli ya dunia ambayo yalifanyika kwenye ardhi ya Afrika, yakivutia waendesha baiskeli mashuhuri Tadej Pogacar na Magdeleine vallieres.
Michezo imekuwa na mchango mkubwa kwa taswira ya Rwanda, ambapo pia Kigali imekuwa mwenyeji wa mashindano ya mpira wa kikapu barani Afrika maarufu kama FIBA na NBA, na inalenga kujaribu kuandaa mashindano ya magari ya Langalanga ‘Formular 1’.
Aidha kampeni yake ya utalii ya “Tembelea Rwanda”, imeendelea kung’ara ambapo imejumuishwa katika jezi za klabu ya Arsenal ya Uingereza na PSG ya Ufaransa.
Hata hivyo licha ya mafanikio haya, rais wa Rwanda, Paul Kagame ameendelea kushutumiwa nchi yake kukithiri kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu, wanaharakati wakitaka mashindano makubwa ya kidunia kutofanyika kwenye taifa hilo.
Mwaka uliopita, shirikisho la kimataifa la mchezo wa baiskeli, lililazimika kukanusha taarifa kuwa mashindano ya dunia yaliyofanyika nchini Rwanda yalikuwa yapelekwe Uswizi kwasababu ya mzozo wa mashariki mwa nchi ya DRC, ambapo Kigali inashutumiwa kushirikiana na waasi wa M23 kutekeleza uasi mashariki mwa nchi hiyo.
Mashindano ya mwaka huu ya Tour du Rwanda 2026 yamevutia waendeshaji baiskeli 84 kutoka timu 17 duniani, hatua ya kwanza ikianzia Rukomo katika Wilaya ya Gicumbi hadi Rwamagana, hii ikiwa njia ndefu zaidi yenye kilometa 173.6.
Leo itakuwa ni hatua ya pili kutoka Nyamata hadi Huye umbali wa kilometa 134.
Matokeo ya jana:
1. Itamar Einhorn (NSN Development Team) – 4h 00’05”
2. Hodei Muñoz (Soudal Quick-Step Devo Team)
3. Mewael Girmay (Istanbul Team)
4. Henok Mulubrhan (Eritrea National Team)
5. Christiaan Rees Van (Development Team Picnic PostNL)