
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imeuonya utawala wa kizayuni wa Israel kwamba hatua yake ya kuzidi kujiingiza ndani ya Mji wa Ghaza kutaugeuza mji huo kuwa “kaburi,” la wanajeshi wa kizayuni baada ya sita miongoni mwao kuangamizwa na wanamuqawama wa Palestina katika matukio tofauti wakati wa jeshi la Israel likiwa linaendeleza mashambulizi makali na ya kinyama yanayolenga kulikalia kwa mabavu eneo lote la Ghaza.
Tawi la kijeshi la Hamas la Izzuddinul-Qassam, limeeleza katika taarifa kwamba Ghaza ni “vita vya msuguano vyenye gharama kubwa” na kuonya kwamba hatima ya mateka wa Israel inategemea harakati za kijeshi za utawala huo wa kizayuni.
Taarifa hiyo ya Al-Qassam iliyotolewa kwa Kiebrania imesisitiza kuwa wapiganaji wa Hamas wamesambazwa katika vitongoji vyote vya Ghaza, wakiwa tayari kukabiliana na jeshi la utawala ghasibu wa Israel.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, mateka wa Israel sasa wametawanywa katika vitongoji katika Mji wa Ghaza na kuonya kwamba vikosi vya Al-Qassam havitawahakikishia usalama wao maadamu Netanyahu angali ameazimia “kuwaua.”
Jana Alkhamisi, askari wa jeshi la utawala wa kizayuni walisonga mbele zaidi kaskazini mwa Ghaza, huku vifaru vya jeshi hilo vikionekana kuelekea katikati ya Jiji la Ghaza, ambapo wakazi wa eneo hilo waliripoti kuvurugika huduma za simu na intaneti.
Wahudumu wa afya wa eneo hilo walisema miili ipatayo 33 ya Wapalestina waliouawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya jeshi la Israel, ilipelekwa katika Hospitali ya Al-Shifa.
Jana hiyohiyo, jeshi la kizayuni lilitangaza kuwa wanajeshi wake wanne waliuawa na wengine watatu walijeruhiwa huko Rafah, kusini mwa Ghaza.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, askari hao waliangamizwa wakati bomu liliporipuka kando ya barabara kwenye njia liliyopita gari aina ya Hummer jeep.
Mbali na tukio hilo, wanajeshi wengine wawili wa Israel walipigwa risasi na kuuawa na mkazi mmoja wa Jordan kwenye kivuko kati ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na nchi hiyo…/