Brazil imewasilisha rasmi ombi la kujiunga katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Israel kuhusu vita vinavyoendelea tangu Oktoba 2023 ambavyo vinatambuliwa na wengi kuwa ni vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Ijumaa, mahakama hiyo yenye makao yake The Hague ilithibitisha kuwa Brasilia iliwasilisha ombi hilo tarehe 17 Septemba, kwa mujibu wa Kifungu cha 63 cha Kanuni ya Mahakama.

Brazil imesema inatekeleza haki yake kama mwanachama wa Mkataba wa 1948 wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari, kabla ya kuwasilisha tamko lake. Brazil imesema utawala wa Israel umekiuka vipengele kadhaa vya mkataba huo.

Afrika Kusini ilianzisha kesi hiyo Disemba mwaka 2023 baada ya utawala wa Israel kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya eneo la pwani la Gaza Oktoba mwaka huo huo. Afrika Kusini inasisitiza kuwa vita vya Israel dhidi ya Gaza vimekiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Pretoria iliwasilisha ushahidi wa kina kwa mahakama kuhusu mauaji ya kimbari. Kufikia Mei, nchi zisizopungua tisa zilikuwa zimewasilisha rasmi au kutangaza nia ya kujiunga na kesi hiyo. Mwezi Juni, Al Jazeera iliripoti kuwa idadi hiyo imefikia nchi 13.

Hivi karibuni, Tume ya Uchunguzi ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ilibainisha kuwa maafisa na vikosi vya utawala huo “wamekuwa, na wanaendelea kuwa na” nia ya mauaji ya kimbar dhidi ya wakazi wa Gaza wanaozidi milioni mbili.

Mashambulizi hayo ya kijeshi yamepelekea Wapalestina takriban 65,200 kupoteza maisha, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, tangu kuanza kwa vita hivyo. Hao ni wale waliopotza maisha moja kwa moja vitani huku taarifa zikisema malaki ya Wapalestina wamepoteza maisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *