
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema, uamuzi wa Baraza la Usalama la umoja huo wa kutoondoa moja kwa moja vikwazo ilivyowekewa Iran unadhoofisha chombo hicho kikuu cha kimataifa, unavuruga diplomasia na unahatarisha Mkataba wa Kuzuia Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT).
Amir Saeid Iravani aliyasema hayo jana Ijumaa baada ya wajumbe 15 wa Baraza la Usalama kupiga kura za kupinga azimio lililotaka kuzuiliwa uwekaji tena wa vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Iran kwa sababu ya mpango wake wa kunufaika na nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.
Iravani alisema, Iran haioni kama ina wajibu wa kutekeleza hatua ya Baraza la Usalama ambayo imechukuliwa kwa “pupa, bila ulazima na kinyume cha sheria”.
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa indhari kwamba dhima kamili ya matokeo hasi ya uamuzi huo itabebwa na Marekani pamoja na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, nchi tatu za Ulaya zilizotia saini makubaliano ya nyuklia ya 2015 – ambayo yanajulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA).
Iravani amebainisha kuwa, Marekani na Troika ya Ulaya zimeibua tuhuma dhidi ya Tehran huku zikiwezesha kutekelezwa mashambulizi ya kihalifu ya utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambavyo vilikuwa vikifanyiwa ukaguzi chini ya makubaliano kamili ya kudhamini usalama yaliyofikiwa kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
“Mpango wa nyuklia wa Iran hautaangamizwa katu kwa bomu, wala kukwamishwa kwa vikwazo na kukengeushwa kwenye mkondo wake wa malengo ya amani,” amesisitiza Iravani.
Aidha, amekumbusha kuwa mlango wa mazungumzo ya kidiplomasia haujafungwa, lakini amesisitiza kwa kusema, ni Iran, na si maadui zake, ndiyo itakayoamua ifanye mazungumzo na nani na kwa msingi gani.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilipiga kura ya kupinga kuondolewa moja kwa moja vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran kwa sababu ya mpango wake wa amani wa nyuklia.
Baraza hilo lenye wanachama 15 halikupitisha rasimu ya azimio iliyoandaliwa na Korea Kusini, kama rais wake, baada ya nchi tisa wanachama kupiga kura za kupinga, dhidi ya nne zilizounga mkono na mbili zilizoamua kutopiga kura, ikimaanisha kurejeshwa tena na nchi za Ulaya vikwazo dhidi ya Iran ifikapo Septemba 28 endapo hakutafikiwa makubaliano ya kimsingi kabla ya wakati huo…/