
Iran imelaani vikali jaribio la mataifa matatu ya Ulaya—Uingereza, Ufaransa na Ujerumani—la kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi yake kupitia kile kinachoitwa utaratibu wa “snapback,” na kuitaja hatua hiyo kuwa “kitendo kisicho halali, kisicho na msingi na cha kichochezi”
Tamko hilo limekuja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura Ijumaa dhidi ya azimio lililopendekezwa la kuondoa kabisa vikwazo vinavyohusiana na mpango wa nyuklia wa Iran. Wanachama tisa walipinga azimio hilo, huku Russia, China, Pakistan na Algeria zikiunga mkono, huku nchi mbili zikijuzuia kupiga kura. Endapo makubaliano hayatafikiwa, vikwazo hivyo vitarejeshwa kufikia Septemba 28.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeeleza kuwa hatua hiyo “inavuruga mchakato wa kidiplomasia unaoendelea” na ni kinyume na sheria za kimataifa. Wizara hiyo imesema, “Vitendo vya kiharibifu vya mataifa matatu ya Ulaya vya kurejesha maazimio ya Baraza la Usalama yaliyokwisha batilishwa vinakuja wakati ambapo vituo vya nyuklia vya Iran vilivyolindwa kisheria vimevamiwa na kuharibiwa katika hujuma za kijeshi za utawala wa Israel pamoja na Marekani.”
Iran imesisitiza kuwa mashambulizi hayo yanakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa, yanatishia amani na usalama wa kimataifa, na yanadhoofisha kwa kiasi kikubwa misingi ya mfumo wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia.
Wizara hiyo imeongeza kuwa, “Mataifa hayo matatu ya Ulaya si tu kwamba hayakulaani mashambulizi ya Israel na Marekani, bali pia yamepelekea kukiukwa mara mbili utaratibu wa kutatua migogoro wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.”
Iran imesitiza kuwa Marekani na mataifa ya E3 ndiyo yanabeba dhamana kamili ya madhara yatakayotokea, kwa kuwa “yamepotosha ukweli, yametoa tuhuma zisizo na msingi, na yamewashinikiza baadhi ya wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama.”
Iran imesisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani na unaakisi matakwa ya wananchi wake ya kuendeleza maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia. Tehran imeahidi kutetea haki zake kupitia njia za kidiplomasia, huku ikihifadhi haki ya kujibu hatua zozote zisizo halali.
Hatimaye, Iran imetoa wito kwa nchi zote zinazowajibika kukataa hatua hiyo ya Ulaya na kutoipa uhalali wowote.
Kwa muda mrefu, Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mataifa ya E3 hayana msingi wa kisheria wa kutumia utaratibu wa “snapback,” hasa ikizingatia ukiukaji wao wa makubaliano ya JCPOA ya mwaka 2015 baada ya Marekani kujiondoa mwaka 2018. Tehran inasema kuwa ilipunguza ahadi zake za nyuklia kama jibu kwa ukiukaji huo.