Makundi mawili ya wanamgambo wa Wazalendo, yanayoongozwa na majenerali wanaojiita Malaika na Nyakiliba, yamekuwa yakipambana tangu Septemba 17 katika eneo la Mwenga, mkoani Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakiwania udhibiti wa mji wa kimkakati.

Mwanaharakati wa kijamii Julius Byemba Kika amenukuliwa na vyombo vya habari akisema: “Watu wasiopungua wanane, wakiwemo raia watatu na wanamgambo watano, wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika mapigano yaliyosababishwa na vizuizi vya barabarani, ambavyo vilitoza ada kubwa kati ya faranga 20,000 hadi 100,000 za Kongo (sawa na dola 7 hadi 36 kwa kila kupita). Mvutano uliongezeka baada ya agizo la kuviondoa vizuizi hivyo kutolewa.”

Haijakuwa rahisi kuwapata wawakilishi wa serikali katika eneo la Mwenga, lakini Foka Mike, kiongozi wa kundi la Wazalendo, amethibitisha vifo hivyo.

Mapigano hayo ya siku mbili yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali na kuongezeka kwa hali ya taharuki.

Wakazi wa Mwenga wanalalamikia masaibu mapya, huku tayari wakikabiliwa na bei za juu za vyakula kutokana na barabara ya RN2 kuwa haipitiki, pamoja na athari za vita vinavyoendeshwa na waasi wa M23. Vizuizi vya barabarani vinaonekana kuwa mzigo wa ziada kwao.

Eneo hilo limekuwa likishuhudia migogoro ya mara kwa mara ya kivita, ikiwemo katika kijiji cha Muhuzi ambako mapigano ya hivi karibuni yalisababisha vifo vya watu kadhaa.

Wakati huohuo, huko Kivu Kaskazini mapigano makali yamezuka kati ya vikosi vya Wazalendo na waasi wa AFC/M23 tangu Ijumaa katika eneo la Osso Banyungu, wilayani Masisi. Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) limeunga mkono operesheni hizo kwa mashambulizi ya anga karibu na Bibwe. Mashuhuda wameripoti milio mizito ya risasi iliyosababisha usumbufu wa usafiri kati ya Nyabiondo na Kashebere na kueneza hofu miongoni mwa raia.

Kundi la waasi la M23 na jeshi la FARDC wanatuhumiana kwa kukiuka makubaliano ya Doha.

Mapigano haya yanaonesha ukubwa wa hali ya ukosefu wa usalama inayozidi kuyumbisha eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri mkubwa wa madini. Inaaminika kuwa mapigano ya mashariki mwa Kongo yanachochewa na madola ya kigeni, hasa ya Ulaya, ambayo yanapora madini yenye thamani wakati wa vita.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *