
Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina imesema, hakuna mapendekezo mapya ya kusitisha vita Ghaza ambayo yamepokelewa hadi sasa na kuongeza kuwa, Marekani na nchi za Magharibi hazitaki kukomesha vita hivyo hadi pale makundi yote ya Muqawama yanayoupinga utawala wa kizayuni wa Israel, -na si Palestina pekee- bali katika eneo lote, yatakapotokomezwa.
Naibu Katibu Mkuu wa harakati hiyo ya Muqawama na ukombozi wa Palestina Mohammad Al-Hindi, amesisitiza kuwa, Israel na Marekani hazijawahi kuwa na nia ya dhati katika mazungumzo, akiashiria kujiondoa kwao kwenye mapendekezo yaliyowasilishwa hapo awali na mjumbe wa Marekani yenyewe Steve Wittkoff, ambayo Muqawama wa Palestina ulishaeleza kuwa umeyakubali.
Aidha, Al-Hindi amekumbusha kuwa utawala wa kizayuni uliushambulia kwa makombora na mabomu ujumbe wa Palestina nchini Qatar ulipokuwa ukijadili pendekezo la kusitishwa mapigano huko Ghaza.
Naibu Katibu Mkuu wa Jihadul-Islami ameielezea hali ya sasa kuwa ni ya “mkwamo” akimaanisha kutokuwepo mapendekezo yoyote mapya yaliyotolewa kwa wakati huu. Ameashiria pia kutambuliwa hivi karibuni Palestina kama nchi-dola na baadhi ya washirika wa Israel wa Ulaya, na kueleza kwamba hatua hiyo ni pigo la kidiplomasia kwa utawala huo wa kizayuni.
Hata hivyo, Al-Hindi ametanabahisha kuwa kutambuliwa huko kutakuwa na taathira ndogo ikiwa hakutapelekea kukomeshwa mauaji ya kimbari huko Ghaza na upanuzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa kizayuni katika Ukingo wa Magharibi.
Afisa huyo wa Muqawama wa Palestina ameziasa nchi za Magharibi na za Kiarabu zitathmini upya hatua yao ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel na kuangalia upya ushirikiano wao wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi na utawala huo unaokalia ardhi za Palestina kwa mabavu…/