Benyamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, amekiri kwamba utawala huu unaishi katika aina fulani ya kutengwa kimataifa.
Netanyahu, amekiri kuzidi kutengwa kwa uchumi wa utawala huo kutokana na kuendelea kwa vita vyake vya jinai huko Gaza.
Yair Lapid, kiongozi wa upinzani wa utawala ghasibu wa Israel amesema kuhusiana na suala hili kwamba hali hiyo inatokana na sera mbovu na zilizofeli za Netanyahu na baraza lake la mawaziri.
Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameandika katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kuwadia mwaka mpya wa Kiyahudi katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X kwamba licha ya madai yake ya ushindi, Benjamin Netanyahu ameiletea Israel uharibifu usio na mfano wake na kutengwa kimataifa.
Araghchi ameongeza kuwa utawala wa kijinai wa Israel haujawahi kuchukiwa kama ilivyo sasa kieneo na kimataifa. Inachukiza kwamba anafanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina kwa jina la Uyahudi na Mayahudi, na hivyo kuchafua sura ya Mayahudi wote duniani.
Kutengwa kwa utawala wa Kizayuni kiuchumi na kimataifa kumeliweka baraza la mawaziri la Netanyahu katika hali ngumu, ambapo makampuni makubwa kimataifa hayana tena hamu ya kuendesha shughuli zao za kibiashara katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
Mashambulio ya kikatili na ya kimbari ya jeshi la utawala wa Kizayuni huko Gaza yameibua wimbi la kulaaniwa kimataifa ambapo nchi na taasisi nyingi zimetoa wito wa kusitishwa ushirikiano na Tel Aviv. Wasanii, wanamichezo na mashirikisho ya michezo ya kimataifa yametoa wito wa kususiwa utawala wa Kizayuni. Vikwazo hivi ni ukumbusho wa kampeni ya kimataifa kama hiyo iliyofanywa kimataifa katika miaka ya nyuma dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Makampuni na Mifuko ya Kifedha ya Magharibi pia imeondoa uwekezaji wao katika makampuni ya Israel. Mashirika ya kutathmini mikopo kama vile Moody’s yameonya dhidi ya kupungua viwango vya mikopo vya utawala wa Kizayuni, jambo ambalo linaweza kupunguza zaidi uwekezaji wa kigeni katika miradi ya utawala huo.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni anakabiliwa na hali ngumu katika kutekeleza malengo yake katika baraza la mawaziri kwa sababu Wazayuni wenye misimamo mikali wanapinga mabadiliko yoyote yatakayopelekea kusimamishwa vita. Baraza la mawaziri la Netanyahu linategemea miungano inayokataa makubaliano ya usitishaji vita, jambo ambalo limesababisha mkwamo wa kisiasa mjini Tel Aviv.
Kutokana na kushadidi msukosuko wa kiuchumi na kuzidi kutengwa utawala wa Kizayuni, zaidi ya watu milioni 2.8 katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hawana chakula cha kutosha ambapo asilimia 32 ya familia zinakosa usalama wa chakula. Katika hali hiyo mashirika ya ndege na maonyesho ya kimataifa pia yanakataa kushirikiana na utawala wa Kizayuni. Mwenendo huo unaonyesha kuwa, kutengwa utawala wa Kizayuni kumeathiri si tu ngazi ya kisiasa bali pia uchumi, utamaduni, michezo na hata maisha ya kila siku katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Mgogoro wa kiuchumi huko Israel ni matokeo ya vita vya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza. Takwimu za taasisi za Kizayuni pia zinaonyesha kuwa, vita vya siku 12 kati ya utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Iran, na operesheni kubwa ya makombora ya Iran pia vimepelekea kuongezeka mdororo wa kiuchumi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Kutengwa utawala wa Kizayuni kiuchumi na kimataifa kumegeuka kuwa mgogoro mkubwa wenye sura nyingi, ambao matokeo yake yanaonekana wazi katika ngazi za kidiplomasia na kibiashara. Hali hiyo imepelekea baraza la mawaziri la Netanyahu kushindwa kabisa kujiondoa katika mzozo wa kiuchumi na mporomoko wa kisiasa.
Siasa za kupenda vita za utawala wa Kizayuni huko Gaza na katika eneo zima la Asia Magharibi zimeacha madhara makubwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na eneo, suala ambalo bila shaka litazidisha kuendelea kutengwa utawala huo haramu wa Kizayuni katika ngazi za kieneo na kimataifa.