
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametuma salamu za pongezi kwa Mfalme, Mrithi wa Kiti cha Ufalme, na wananchi wa Saudi Arabia katika maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya ufalme huo.
Katika ujumbe tofauti aliowatuma Jumanne kwa Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud na Mrithi wa Kiti cha Ufalme Mohammed bin Salman, Rais Pezeshkian amesisitiza dhamira ya kuendeleza uhusiano uliorejeshwa kati ya mataifa haya mawili ya kikanda.
Katika ujumbe wake kwa Mfalme wa Saudi Arabia, Rais Pezeshkian alitaja uhusiano wa kihistoria na kitamaduni uliopo kati ya mataifa hayo, akieleza matumaini yake kuwa mahusiano ya pande mbili yataendelea kupanuka katika nyanja mbalimbali.
Alibainisha kuwa: “Mambo mengi yanayofanana kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ufalme wa Saudi Arabia ni msingi imara wa urafiki kati ya mataifa haya mawili ya Kiislamu na yanadumisha uhusiano wa pamoja.”
Katika ujumbe wake kwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Rais wa Iran ameelezea matumaini yake kuwa kupitia juhudi za pamoja na “matumizi ya hali ya juu ya uwezo uliopo,” mataifa haya mawili yataona upanuzi mkubwa wa ushirikiano katika “nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.”
Siku ya Kitaifa ya Saudi Arabia ni sikukuu ya umma inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Septemba, kuenzi tangazo la kifalme la mwaka 1932 lililobadilisha jina la Ufalme wa Nejd na Hijaz kuwa Ufalme wa Saudi Arabia, chini ya amri ya Mfalme Abdulaziz ibn Saud.