Kwa mara ya kwanza, Wizara ya Usalama ya Iran imeonyesha hadharani picha na taswira nyeti za ndani ya kinu cha nyuklia cha Dimona cha utawala wa kizayuni wa Israel.

Taswira hizo ni ithibati ya kushindwa na kufeli kiintelijensia utawala haramu wa Israel, na namna Iran ilivyofanikiwa kupenya ndani kabisa ya utawala huo kupitia oparesheni tata na ya utaalamu wa hali ya juu.

Waziri wa Usalama wa Iran Ismail Khatib amezielezea taarifa zilizonaswa kuwa ni hazina ya kiintelijensia ya silaha za Israel na akasema: “hazina hiyo iliyohamishiwa nchini inajumuisha mamilioni ya kurasa za taarifa mbalimbali na zenye thamani kubwa zinazohusiana na utawala wa Kizayuni”.

Filamu ya matukio halisi iitwayo “Pango la Buibui” (The Spider’s Lair) ambayo ilionyeshwa jana usiku Septemba katika televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni simulizi ya namna maajenti wa ujasusi wa Iran walivyoweza kunasa na kuhodhi hazina ya taarifa za silaha za utawala wa Kizayuni pamoja na orodha ya wahakiki, watafiti na maafisa waandamizi wa miradi ya silaha zinazokinzana na ubinadamu wakiwemo pia wa wanasayansi wa Marekani na Ulaya wanaohusika na miradi hiyo.

Kwa mujibu wa Ismail Khatib, wakati wa Vita vya Siku 12 katika mwezi wa Juni, baadhi ya vituo hivyo vililengwa na vitengo vya makombora vya Iran baada ya taarifa zake zote kukusanywa pamoja kupitia kwenye nyaraka hizo.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa kwenye filamu ya Pango la Buibui, ndani ya hazina hiyo ya taarifa za kiintelijensia zilizohamishiwa humu nchini kuna picha na taswira nyeti ilizonasa Wizara ya Usalama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za makazi ya Waziri wa Vita wa Israel, taswira maalumu za ndani ya kinu cha nyuklia cha Dimona kilichoko ndani ya Israel, picha zilizovuja za Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na mamilioni ya kurasa za taarifa mbalimbali za kiintelijensia zinazohusiana na utawala huo wa kizayuni…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *