
Mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Syria Tom Barrack amedai kuwa utawala wa kizayuni wa Israel na Syria zinakaribia kufikia makubaliano ya usalama.
Barrack ametoa matamshi hayo huku Marekani ikiwa inashinikiza kukamilishwa makubaliano ya usalama kati ya pande hizo mbili huko mjini New York.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Kizayuni ya i24 News, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Syria amedai kuwa, Damascus na Tel Aviv zinakaribia kusaini makubaliano ya “kupunguza mvutano”, ambapo utawala wa kizayuni utasimamisha mashambulizi yake dhidi ya Syria, nayo Syria itahakikisha haiweki vifaa na zana nzito za kivita karibu na mpaka wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliyopachikwa jina bandia la Israel.
I24 News imeandika kwamba, matamshi hayo yametolewa saa chache baada ya chombo hicho cha habari kuripoti kwamba “kuna uwezekano mkubwa” waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atakutana na rais wa serikali ya mpito ya Syria, Al-Jolani (Ahmad Al-Sharaa), wiki ijayo mjini Washington.
Siku ya Jumanne, Barak aliwaambia waandishi wa habari kando ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York kwamba makubaliano hayo ya ‘kupunguza mvutano’ kati ya Israel na Syria ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye mapatano ya kiusalama ambayo hivi sasa yanaendelea kujadiliwa na pande hizo mbili.
Mjumbe huyo wa Marekani katika masuala ya Syria ameongeza kuwa, anachotaka Trump ni Tel Aviv na Damascus kufikia makubaliano ambayo yatatangazwa wiki hii, lakini hadi sasa hazijapigwa hatua za kutosha, na mapumziko ya Mwaka Mpya wa Kiyahudi katika wiki hii nayo pia yamezorotesha mchakato huo.
Endapo yatasainiwa, hayo yatakuwa ni makubaliano ya kwanza rasmi kufikiwa kati ya utawala wa kizayuni wa Israel na Syria baada ya miongo kadhaa…/