
Tovuti ya habari ya Politico imeripoti kuwa, katika mkutano wa faragha aliofanya Rais wa Marekani Donald Trump na viongozi wa nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu, rais huyo wa Marekani aliwaahidi viongozi hao kwamba, hatamruhusu waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu autwae kikamilifu Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo.
Ripoti hiyo ya Politico imevitaja vyanzo sita vyenye taarifa za yaliyojadiliwa katika mkutano huo huku “watu wawili kati ya hao wakisema Trump alikuwa thabiti juu ya mada hiyo na kwamba rais aliahidi kuwa Israel haitaruhusiwa kuutwaa kikamilifu Ukingo wa Magharibi”.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo ya habari, Trump aliwasilisha kwenye mkutano huo na viongozi wa nchi za Kiislamu waraka wa mwongozo juu ya namna ya kumaliza vita vilivyoanzishwa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Ghaza, ambao unajumuisha ahadi ya kuzuia kunyakuliwa Ukingo wa Magharibi na mpango wa utawala na usalama wa Ghaza baada ya vita.
Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema, ahadi hiyo iliyotolewa na Trump inaonekana ni kitu cha kushangaza ikizingatiwa kwamba sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu tayari imeshaporwa na Israel na viongozi wa Marekani wameunga mkono hatua hiyo hadharani au kuipa mgongo na kutoijadili.
Kuhusiana na mkutano wa rais wa Marekani na viongozi wa nchi za Kiislamu, ni Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki pekee ndiye aliyetoa maoni yake hadharani akisema majadiliano hayo yalikuwa “chanya na yamezaa matunda”, lakini hadi sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu kile kilichojadiliwa.
Mkutano huo wa faragha uliofanyika siku ya Jumanne pembeni ya mkutano wa Umoja wa Mataifa ulihudhuriwa na Trump na viongozi kutoka Uturuki, Qatar, Saudi Arabia, Misri, Pakistan, Jordan, Indonesia na Muungano wa Falme za Kiarabu…/