Rais wa Kenya William Ruto ametoa hotuba kali katika kikao cha 80 cha Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York siku ya Jumatano.

Katika hotuba yake hiyo, Ruto amegusia masuala mbalimbali ikiwemo hali mbaya ya mafaa wanayoishi nayo Wapalestina wa Ghaza, vita vya Sudan, haja ya mabadiliko ya kitaasisi katika Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa za fedha kama vile IMF na Benki ya Dunia, hali ya usalama nchini Haiti, na taharuki za kisiasa zinazoshuhudiwa duniani kote.

Kuhusiana na hali ya Ghaza, Rais wa Kenya amesema, nchi yake inatiwa ‘wasiwasi mkubwa’ na janga baya linaloshuhudiwa katika eneo hilo na kutoa wito wa kusitishwa kikamilifu mapigano na kuheshimiwa sheria ya kimataifa.

“Ni kwa kupitia mchakato huo tu ndiyo dira ya kupatikana kwa suluhu ya mataifa mawili itafikiwa — ambapo Israel na Palestina watakuwa majirani, kwa amani na usalama”, ameeleza kiongozi huyo.

Katika hotuba yake hiyo mbele ya hadhara ya nchi zote wanachama wa UN, Ruto amezungumzia pia mabadiliko ya kimuundo ya Umoja wa Mataifa hususan Baraza la Usalama la umoja huo na kusisitizia udharura wa Afrika kuwa na viti viwili vya kudumu katika baraza hilo na kuwa na uwezo wa kura ya turufu, mbali na nafasi zingine zisizo za kudumu.

Rais wa Kenya amebainisha kuwa mabadiliko ya Umoja wa Mataifa hayamaanishi kuwa ni “kuifanyia fadhila Afrika”, bali ni jambo la lazima kwa taasisi hili ili kuendelea kuwa na maana.  

Amekumbusha kuwa, sehemu kubwa ya ajenda za Baraza la Usalama huwa ni kuhusu Afrika, lakini ndilo bara pekee ambalo halina uanachama wa kudumu kwenye baraza hilo linalopitisha maamuzi kuhusu hatima ya nchi za bara hilo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ruto amezishutumu taasisi za fedha za kimataifa kama vile IMF na Benki ya Dunia kwa “kutoonyesha usawa kwa Afrika”. Amesema, taasisi hizo zinaonekana kutoa fedha zaidi kwa mataifa tajiri huku “zikiiadhibu” Afrika kwa riba kubwa, viwango vidogo vya mikopo na masharti mengi sana…/ 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *