Ikulu ya Kremlin imetangaza kuwa Russia haina “mbadala” isipokuwa kuendelea kupigana vita, huku ikijibu mapigo kwa mabadiliko ya ghafla yaliyoonyeshwa dhidi ya nchi hiyo na Rais wa Marekani Donald Trump mkabala wa Ukraine kwa kufikia hadi ya kuiita Moscow “chui wa karatasi”.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amejibu mapigo kwa madai ya Trump kwamba Ukraine inaweza kushinda vita hivyo, na kusisitiza kwamba Russia itaendeleza mashambulizi yake dhidi ya Ukraine ili ‘kulinda maslahi yake na kufikia malengo yake’.

“Tunafanya hivi kwa ajili ya sasa na kwa mustakabali wa nchi yetu. Kwa vizazi vingi vijavyo. Kwa hiyo, hatuna njia mbadala,” amesisitiza Peskov katika mahojiano ya redio na kituo cha redio cha RBC cha Russia.

Siku Jumanne Trump alibadili msimamo wake kwa kuiunga mkono kikamilifu Ukraine baada ya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelenskyy kando ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alipoweka ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii akisema nchi hiyo “iko katika nafasi ya kupigana na KUSHINDA na kurejesha Ukraine yote katika hali yake ya awali”.

Akiashiria kumalizika ukuruba uliokuwepo kati yake na Russia, rais huyo wa Marekani alisema: “Russia imekuwa ikipigana bila malengo kwa miaka mitatu na nusu, vita ambavyo vilipaswa kuifanya Nguvu Halisi ya Kijeshi ichukue chini ya wiki moja kushinda” na akaongezea kwa kusema vita hivyo vimeifanya Russia ionekane kama “chui wa karatasi” ikiwa na uchumi uliodorora.

Akijibu mapigo kwa kauli hiyo ya Trump, msemaji wa Kremlin amesisitiza kuwa nchi hiyo iko zaidi ya “dubu” zaidi. Amesema ni makosa kufikiria kuwa Ukraine inaweza kutwaa tena ardhi iliyochukuliwa na jeshi la Moscow.

Aidha, Peskov amelibeza jaribio la Trump la kutaka kukaribiana na Russia kwa kumkaribisha rais wa nchi hiyo Vladimir Putin kwa mkutano maalumu huko Alaska mwezi uliopita, akisema matokeo ya mkutano huo “yamekaribia sifuri”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *