Takriban raia 15 wameuawa na wengine 12 kujeruhiwa katika shambulio la droni na ndege zisizo na rubani linalodaiwa kufanywa na RSF kwenye soko moja ndani ya mji wa El Fasher wa magharibi mwa Sudan.

Afisa mmoja wa “Hospitali ya Saudi” huko el Fasher ameviambia vyombo vya habari kwamba hospitali hiyo imepokea majeruhi wengi. Amesema: “Kwa mujibu wa hesabu yetu, watu 15 wameuawa na wengine 12 wamejeruhiwa.”

Afisa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa sababu si msemaji rasmi wa hospitali hiyo pia amesema: “Wengi wa waliojeruhiwa wako katika hali mbaya na wanahitaji hatua za haraka za upasuaji. Hali ni mbaya kutokana na uhaba mkubwa wa vifaa tiba na wafanyakazi waliobobea kwenye masuala makubwa kama hayo.”

Wakati huo huo kikundi kimoja cha kujitolea huko El Fasher kwa kifupi CRC kimeripoti kuwa, droni na ndege zisizo na rubani za RSF zilishambulia soko moja lenye msongamano wa watu katika mji huo juzi Jumanne na kusababisha watu 27 kuuawa na kujeruhiwa.

Tangu Mei 10, 2024, mapigano makali yamekuwa yakiendelea huko El Fasher kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na washirika wao kwa upande mmoja, na RSF kwa upande mwingine, huku mapigano yakizidi kuwa makali na makubwa, siku baada ya siku.

Uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi umeitumbukiza Sudan kwenye mzozo mkubwa kati ya makundi mawili ya kijeshi, ya SAF na RSF, tangu mwezi Aprili 2023. Mapigano hayo yameshaua makumi ya maelfu ya watu na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *