Rais wa Marekani Donald Trump amezituhumu India na China kuwa “zinafadhili kifedha” vita vya Ukraine kupitia uagizaji wa nishati kutoka Russia. Trump ametoa shutuma hizo katika hotuba yake kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York.

Huko nyuma Trump alitetea mpango wa kuyawekea vikwazo vidogo mataifa yanayoendeleza uhusiano wa kiuchumi na Russia ili kuongeza mashinikizo ya kifedha dhidi yao. Beijing na New Delhi zote mbili ziliielezea mbinu hiyo ya Marekani kuwa ni kitu kisichokubalika na kukataa kusalimu amri mbele ya shinikizo hilo.

“China na India ndio wafadhili wakuu wa vita vinavyoendelea kwa kuendelea kununua mafuta ya Russia”, alidai Trump katika hotuba yake hiyo.

Rais wa Marekani aliwakejeli pia wanachama wa shiriki la kijeshi la NATO wanaoendelea kuagiza mafuta na gesi ya Russia akisema, wao kwa hakika “wanafadhili vita dhidi yao wenyewe” kwa kununua nishati kutoka Russia huku wakati huo huo wakiwa “wanapambana na Russia.”

Mapema mwezi huu, Trump aliutaka Umoja wa Ulaya uanze kuziwekea ushuru wa hadi 100% bidhaa za India na China. Hata hivyo, pendekezo hilo lilipingwa na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, ambaye alisema umoja huo “utajichukulia wenyewe maamuzi ya kufanya.”

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, Washington iliweka ushuru wa adhabu wa 25% dhidi ya India, na kuufanya ushuru dhidi ya bidhaa za nchi hiyo ufikie 50% ikiitaja sababu ya kuchukua hatua hiyo kuwa ni kushindwa New Delhi kupunguza ununuzi wa mafuta kutoka Russia. Marekani bado haijawekea ushuru wowote mpya China, baada ya vita vya ushuru vilivyozuka kati ya pande hizi mbili mapema mwaka huu kufikia kwenye usitishaji wa muda…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *