
Balozi wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni anatarajiwa kuelekea Cairo mji mkuu wa Misri hivi karibuni ili kuwasilisha mpango wa rais wa Marekani wa eti kukomesha vita vya Ghaza.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Mike Huckabee anapanga kuelekea Cairo katika siku zijazo kwa madai ya kupunguza “mivutano” baina ya Misri na utawala wa Kizayuni na kujadili mpango wa Trump wa eti kumaliza vita vya Ghaza.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Huckabee atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty katika safari yake hiyo ili kuhakiki undani wa mpango wa Trump wa eti kumaliza vita dhidi ya Ghaza.
Huckabee pia atajadiliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, kile kinachodaiwa ni mvutano wa kidiplomasia kati ya Tel Aviv na Cairo hususan baada ya Misri kuonesha wasiwasi mkubwa kuhusu mpango wa Israel wa kuwahamishia Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza kwenye ardhi ya Misri.
Utawala wa Kizayuni una wasiwasi pia na Misri kutokana na Cairo kuimarisha jeshi lake katika Rasi ya Sinai hasa baada ya Israel kufanya shambulio la kigaidi mjini Doha, Qatar.
Gazeti la Haaretz la utawala ghasibu wa Israel limezinukuu duru za kidiplomasia zikisema kuwa, mazungumzo ya balozi huyo wa Marekani huko Cairo yatatathmini upya pia mapatano makubwa ya gesi baina ya utawala wa Kizayuni na Misri. Hivi karibuni, Misri na utawala wa Kizayuni zilitiliana saini makubaliano makubwa ya kuuziwa Misri gesi ya wananchi wa Palestina ambayo Israel inaiiba kila leo.