
Rais Masoud Pezeshkian amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kwa dhati kupanua ushirikiano wa kina na nchi za Afrika, kwa mujibu wa sera yake ya “diplomasia yenye mlingano” na msisitizo wa maslahi ya pamoja.
Akizungumza katika mkutano na Waziri wa Ulinzi na Masuala ya Maveterani wa Burkina Faso, Brigedia Jenerali Célestin Simporé, mjini Tehran siku ya Jumatatu, Rais Pezeshkian amesema Iran iko tayari kutumia uwezo wake mpana ili kuimarisha uhusiano na mataifa ya Afrika, akisisitiza kuwa hili ni kipaumbele cha kimkakati katika sera yake ya masuala ya kigeni.
Rais wa Iran ameipongeza Burkina Faso kwa msimamo wake wa kimsingi na chanya kuhusu Iran katika majukwaa ya kimataifa, na akasisitiza umuhimu wa kubadilishana ujumbe wa ngazi za juu katika nyanja za kisiasa, ulinzi na uchumi kati ya nchi hizo mbili.
Ameongeza kuwa: “Kuendeleza ziara rasmi na kupanua mashauriano ya kitaalamu kunaweza kufungua njia ya kujenga uaminifu wa kina zaidi, kuimarisha udugu wa kirafiki, na kuongeza kiwango cha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kisayansi, viwandani na kiulinzi.”
Ameongeza kuwa ana imani maendeleo ya uhusiano kati ya Iran na Burkina Faso yatasaidia pia kuinua kiwango cha ushirikiano kati ya Iran na mataifa mengine ya Afrika.
Rais Pezeshkian pia ameusifu moyo wa kutafuta uhuru na msimamo wa kupinga ubeberu wa serikali na wananchi wa Burkina Faso, akisema kuwa nchi hiyo ya Afrika itashinda vita dhidi ya ugaidi kwa kutegemea irada ya taifa na mshikamano wa ndani.
Kwa upande wake, Brigedia Jenerali Simporé ameipongeza Iran kwa msimamo wake thabiti dhidi ya vikwazo kwa kipindi cha zaidi ya miongo minne.
Amesema maendeleo ya Iran katika nyanja za ulinzi na teknolojia za hali ya juu ni ishara ya nguvu ya taifa, kujitegemea kimkakati, na uongozi wenye busara.
Nguvu za kibeberu, amesema, hulenga kuyaweka mataifa katika utegemezi na kuyazuia kufikia mamlaka kamili ya kweli. Waziri huyo wa Burkina Faso ameongeza kuwa wahusika wanaochochea machafuko na ukosefu wa usalama barani Afrika ni hao hao wanaojaribu kulazimisha taifa la Iran kujisalimisha.
Amesema Burkina Faso imekabiliwa na ugaidi na hali ya kutokuwepo kwa utulivu kwa zaidi ya muongo mmoja, lakini akasisitiza kuwa wananchi wa nchi hiyo wameazimia kuendelea na njia ya uhuru, maendeleo ya kijamii, na ustawi wa kiuchumi.