Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Rais Trump wakatahadharisha kwamba Israel italazimika kuimaliza kazi iliyoianzisha kwenye eneo hilo ya kuliangamiza kundi la Hamas ikiwa wanamgambo hao wa Kipalestina wataukataa.

“Lakini kama Hamas wataukataa mpango wako mheshimiwa rais au kama wataukubali kisha kimsingi wafanye kila kitu kuuvunja, basi Israel itamaliza kazi yenyewe, hili linaweza kufanywa kwa njia rahisi ama ngumu, lakini litafanyika. Malengo haya yote lazima yatimizwe kwa sababu hatukupigana vita hivi ili Hamas wabaki Gaza na kututishia tena” alisema Netanyahu.

Hamas bado haijasema chochote kuhusu pendekezo hilo lililotangazwa na Trump kwenye Ikulu ya White House sambamba na Netanyahu na kuacha sintofahamu kuhusiana na mustakabali wake. Mpango huo unatoa miito ya kusitisha mapigano kuachiliwa mateka wanaozuiwa na Hamas katika kipindi cha masaa 72, kuwanyanga’anya silaha Hamas na Israel kuondoka kwa awamu huko Gaza na kufuatiwa na mamlaka ya mpito ya baada ya vita itakayoongozwa na Trump mwenyewe.

Uingereza, Canada na Australia watambua Dola la Palestina

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Trump amshukuru Netanyahu kwa kuukubali mpango wa amani

Kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao, Trump pamoja na mambo mengine alimshukuru Netanyahu kwa kukubaliana na pendekezo hilo ambalo alisisitiza linahusu amani na utulivu wa kikanda.

Alisema “Napenda pia kumshukuru Waziri Mkuu Netanyahu kwa kukubaliana na mpango huu na kuwa na imani kwamba kama tukishirikiana tunaweza kufikisha mwisho vifo na uharibifu tulioushuhudia kwa miaka mingi, miongo na pengine hata kwa karne na kufungua ukurasa mpya wa usalama, amani na utulivu kwenye Ukanda mzima

Trump aidha amesema ataanzisha Baraza la amani litakaloongozwa na yeye mwenyewe na litakalosimamia kipindi cha mpito cha baada ya vita. Akawataja wengine watakaohusika na baraza hilo kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani wa uingereza Tony Blair, aliyemuelezea kama ‘mtu mzuri sana.’

Israel inapakana na Gaza 2025 | Kifaru cha Israel kikiwa kwenye mpaka na Ukanda wa Gaza
Kifaru cha Israel kinasogea kwenye mpaka wa Israel na Ukanda wa Gaza, Septemba 25, 2025, huku kukiwa na vita vinavyoendelea kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas.Picha: Jack Guez/AFP

Sintofahamu kwa upande wa Hamas

Licha ya Hamas kusalia kimya, lakini afisa mmoja mwandamizi aliliambia shirika la habari la AFP kwamba watajibu mara baada ya kulipata pendekezo hilo ingawa afisa mwingine alisema tayari wasuluhishi wa Qatar na Misri waliwasilisha pendekezo hilo kwa Hamas. 

Mataifa manane ya Kiarabu na Kiislamu ya Misri, Jordan, Saudi Arabia, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uturuki, Indonesia na Pakistan yamesifu juhudi za kweli za Trump na kukaribisha mpango huo wa amani kwa ajili ya Gaza. Mataifa hayo yamesema kwenye taarifa ya pamoja kwamba wanaikaribisha hatua hiyo na kuthibitisha utayari wao wa kushirikiana na Marekani na pande nyingine ili kuhakikisha kunafikiwa makubaliano na yanatekelezwa.

Mamlaka ya Palestina iliyojikita Ukingo wa Magharibi na ambayo inajiandaa kwa uongozi wa baada ya vita pia imekaribisha hatua hiyo na kusifu juhudi za Trump huku ikiahidi kufanya mageuzi sawasawa na matakwa ya Marekani.

Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya Antonio Costa kwa upande wake ameziomba pande zinazovutana kutumia fursa hii kupata amani, huku pia akiukaribisha mpango huo akisema hali ya Gaza haivumiliki, huku Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer akiwataka Hamas kukubaliana na mpango huo ili kumaliza hali tete kwa kusitisha vita na kuwaachilia mateka.

Lakini bado vizingiti vingalipo kwa pande zote mbili, na hasa wakati maelezo ya kina yatakapokuwa yakijadiliwa. Na Netanyahu naye huenda akakabiliwa na kizingiti wakati atakapokuwa akiwashawishi wanasiasa wa mrengo wa kulia wa baraza lake la mawaziri kuhusu mpango huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *