Jaji wa Kimarekani amekadhibisha tuhuma dhidi ya UNRWA kwamba inaiunga mkono harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas.

Jaji huyo wa nchini Marekani ametupilia mbali shauri la baadhi ya Waisraili waliolihutumu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) kwamba liliipatia Hamas msaada wa fedha wa zaidi  ya dola bilioni moja na kwamba harakati hiyo ilihusika katika operesheni ya Oktoba 7, 2023.

Analisa Torres Jaji wa Mahakama katika eneo la Manhattan nchini Marekani ameeleza kuwa  UNRWA ina kinga kamili dhidi ya shauri hilo kwa sababu ni shirika tanzu la Umoja wa Mataifa, ambapo mashauri kama haya hayawezi hayawezi kuwasilishwa dhidi yake. Jaji huyo aidha amepinga hoja ya Wazayuni kwamba UNRWA ni taasisi maalumu na haina haki ya kupewa kinga. Jaji huyo amenukuu kauli za wanasheria wa Umoja wa Mataifa waliosema kuwa mashirika tanzu kama vile UNRWA hayako huru kikamilifu kwa sababu taasisi mama zinaweza kubadili muundo au kulifunga shirika hilo tanzu.

Jaji, Analisa Torres 

Bunge la utawala wa Kizayuni (Knesset) Okotoba 27 mwaka 2024 lilipasisha sheria ambayo kwa mujibu wake ni marufuku kutekelezwa shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa KIpalestina (UNRWA) ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Rasimu ya sheria hii tajwa ilipasishwa kwa kura za ndio 92 mkabala wa kura 10 za hapana. Utawala wa Kizayuni ulichua hatua hii lengo likiwa ni kushadidisha mashinikizo kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza. Utawala wa Kizayuni kwa miaka kadhaa sasa umekuwa ukitoa mashinikizo kwa UNRWA; mashinikizo ambayo yameshtadi sambamba na kuanza vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza. Weledi wa mambo wanasema kuwa, UNRWA ni uti wa mgongo wa maisha ya wakimbizi wa Kipalestina, na uamuzi wa hivi karibuni wa Israel wa kupiga marufuku shughuli za shirika hilo utaathiri pakubwa maisha ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.

UNRWA katika Ukanda wa Gaza 

Inaonekana kuwa, moja ya sababu iliyoipelekea Israel kusimamisha shughuli za shirika la UNRWA ni Tel Aviv kudhani kwamba kwa kusimamisha shughuli za UNRWA kadhia ya wakimbizi wa Kipalestina itasahaulika na kufikia kikomo na pia suala la kuasisi nchi huru ya Palestina, suala ambalo  limetamkwa wazi  na viongozi wa Israel.

Nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja kwa mara nyingine tena zimetahdharisha utawala wa Kizayuni kuhusu kupasisha sheria hiyo baada ya indhari iliyotolewa na Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika uwanja huu. 

Utawala wa Kizayuni unadai kuwa kuna mfungamano mkubwa kati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas)  na UNRWA; na kwamba utawala huo hauafiki jambo hilo. Madai haya yasiyo na msingi ya Israel yamepelekea baadhi ya nchi za Magharibi kusitisha misaada yao ya kifedha  wa shirika hilo la kimataifa kwa miezi kadhaa sasa.

Shirika la UNRWA lilianzishwa mwaka 1949 kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina katika nchi mbalimbali  duniani na hasa shirika hilo limekuwa likisimamia vituo vya afya na shule huko Gaza na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Shirika hilo ni uti wa mgongo wa usambazaji misaada ya kimataifa huko Gaza eneo ambalo hivi sasa limekumbwa na maafa ya binadamu yaliyosababishwa na jinai za kinyama za Israel. 

Baada ya kuanza vita dhidi ya Gaza miaka miwili iliyopita, moja ya kadhia muhimu sana za kisiasa na vyombo vya habari katika uga wa kimataifa ni tuhuma za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA. Shirika hili la kimataifa ambalo tangu mwaka 1949 hadi sasa limekuwa na jukumu la kuwasaidia mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina huko Gaza, katika Ukingo wa Magharibi, Lebanon, Syria, na Jordan mara kadhaa limelengwa na mashambulizi ya kipropaganda na kisiasa ya Tel Aviv.

Hii ni katika hali ambayo, moja ya jitihada kubwa zilizofanywa na utawala wa Kizayuni ilikuwa ni kuwatuhumu baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA kwamba wamekuwa wakishirikiana na makundi ya muqawama ya Palestina; tuhuma ambazo zimekabiliwa na mjibizo na radiamali kubwa ya fikra za waliowengi, vyombo vya habari na hata baadhi ya serikali za Magharibi. Pamoja na hayo, baada ya kufanyika uchunguzi huru na kutolewa ripoti mbalimbali kimataifa; ilitangazwa kuwa madai haya ya Israel hayana msingi wowote na UNRWA ikaondolewa mashtaka. Suala hili kwa mara nyingine tena limedhihirisha kuwa utawala wa Kizayuni unalenga kuendesha vita vya kisaikolojia na kipropaganda dhidi ya taasisi zinazoiunga mkono Palestina, badala ya kutaka kuwasilisha ushahidi wa kweli na wenye mashiko. 

Hatimaye, kutupiliwa mbali  mashtaka dhidi ya UNRWA, ambapo kadhia ya karibuni kabisa ilikuwa ni kitendo cha Jaji wa Marekani kutupilia mbali shauri la Wazayuni si tu  ni ushindi wa kisheria au wa vyombo vya habari, bali ni sehemu ya vita vya simulizi kati ya Palestina na Israel; vita ambavyo ndani yake suala la uhalali, fikra za waliowengi na itibari ya kimataifa vina umuhimu mkubwa kuliko silaha za kijeshi. Inaonekana kuwa kushindwa huku kwa Tel Aviv kumeweka wazi mwanya mkubwa kati ya madai na uhakika wa mambo hivyo kutoa fursa kwa mara nyingine tena ya kupazwa sauti ya Wapalestina duniani. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *