London, England. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema nahodha wa timu yake, Martin Odegaard pamoja na kiungo Declan Rice walioshindwa kuendelea katika mechi dhidi ya West Ham wamepata majeraha ambayo yanaonekana  sio mazuri na sasa madaktari wataenda kuwafanyia vipimo zaidi.

Odegaard amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha na katika mechi mbili mfululizo za ligi amekuwa akitolewa katika kipindi cha kwanza kutokana na kushindwa kuendelea.
Aliikosa pia mechi dhidi ya Manchester City kutokana na tatizo la bega.

Inaelezwa staa huyu atakosa mechi kadhaa kutokana na jeraha la goti alilopata katika mechi dhidi ya West Ham ambapo pia Rice aliumia na kushindwa kuendelea katika dakika za mwishoni kipindi cha pili.

“Odegaard aliumia baada ya kugongano goti kwa goti, alihisi maumivu na bado tunasubiri taarifa zaidi kutoka kwa daktari lakini jeraha linaonekana kuwa baya. Amekuwa na bahati  mbaya tangu kuanza kwa msimu huu, amekuwa akusumbuliwa na majeraha mbalimbali mara bega leo ni goti,”alisema Arteta.

“Tutalazimika kuona kiwango cha jeraha kilivyo na kupata suluhisho lakini ni wazi akikaa nje itakuwa ni pigo kwetu kwa sababu ni nahodha wetu na ni mchezaji anayetuongezea kitu cha utofauti  hasa katika mashambulizi. Kwa upande wa  Declan, alikuwa na maumivu ya mgongo. Aliomba kutoka mwenyewe.”

Rice ambaye alitolewa dakika ya 78 baada ya kuanguka na kupatiwa matibabu, alifunga bao moja katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Arsenal kushinda kwa mabao 2-0 na Arsenal kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi.

Ikiwa atakutwa na jeraha kubwa zaidi, Rice ambaye  amekuwa mchezaji tegemeo wa Arsenal anaweza akashindwa kujiunga na timu ya taifa ya England ambayo itakuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya Wales,  Alhamisi kabla ya mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Latvia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *