London, England. Ushindi wa Arsenal dhidi ya West Ham juzi ulikuwa wa kipekee kwa Bukayo Saka, kwani alifunga bao lake katika mechi yake ya 200 ya Ligi Kuu ya England (Premier League).

Winga huyo alicheza kwa mara ya kwanza kwenye ligi hiyo Januari Mosi 2019, na sasa amefikisha michezo 200 chini ya miaka sita. Akiwa bado na umri wa miaka 24, Saka ni mchezaji wa sita mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Arsenal kufikia idadi hii ya mechi, na wa pili katika enzi ya Premier League akitanguliwa tu na Cesc Fabregas.

Katika mechi hizo 200, Saka ameanza michezo 181 na kuingia kama mchezaji wa akiba mara 19.  Amehusika katika ushindi wa mechi 115, sare 41 na kupoteza 44. Anakuwa mchezaji wa 18 wa Arsenal kufikia alama hii katika enzi ya Premier League, na wa 79 katika historia ya klabu kushiriki mechi 200 za ligi.

Katika historia ya Premier League, Saka pia ni wa sita kwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufikia mechi 200 tangu ligi hiyo ilipoanzishwa mwaka 1992, na ndiye aliyefanikisha hili kwa kasi zaidi tangu Raheem Sterling (mchezaji wa zamani mwenzake) alivyofanya hivyo Oktoba 2018.

Katika kipindi hicho, Bukayo amefunga mabao 55 na kutoa pasi za mabao 45, na bao lake kupitia penalti dhidi ya West Ham lilimfanya afikishe jumla ya ushiriki wa mabao 100 (magoli + asisti) katika mechi 200.

West Ham ni wapinzani anaowapenda zaidi katika ligi, kwani amewafunga mabao mengi zaidi (5) kuliko timu nyingine yoyote, na pia kutoa asisti nne idadi ya pili kubwa zaidi baada ya dhidi ya Southampton (5).

Tangu alipoanza kucheza dhidi ya Fulham Januari 2019, ni wachezaji wanane tu waliotoa mchango wa mabao (magoli na asisti) zaidi kuliko Saka katika ligi hiyo.

Bukayo sasa anakuwa mchezaji wa nane wa Arsenal kufikisha ushiriki wa mabao 100 katika Premier League, na Mwingereza wa tatu kufanya hivyo baada ya Ian Wright (123) na Theo Walcott (108). Pia ni mchezaji wa saba mwenye umri mdogo zaidi katika ligi kufanikisha hili na wa kwanza kwa umri mdogo tangu Romelu Lukaku alivyofanikisha hilo Februari 2017.

Wachezaji wa Arsenal waliohusika katika mabao mengi zaidi kwenye Premier League:

Thierry Henry – 249

Dennis Bergkamp – 181

Robin van Persie – 135

Ian Wright – 123

Theo Walcott – 108

Cesc Fabregas – 105

Robert Pires – 103

Bukayo Saka – 100

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *