Nyota wa JKT Queens wameteka kikosi cha timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ kinachojiandaa na mechi mbili za kuwania Kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 dhidi ya Ethiopia baadaye mwezi huu kutokana na kuteuliwa kwa idadi kubwa kulinganisha na timu nyingine.

Kati ya wachezaji 25 walioitwa kikosini na Kocha Mkuu, Bakari Shime, wachezaji 12 ni wa JKT Tanzania ikifuatiwa na Simba Queens ambayo wachezaji wake watatu wameitwa katika kikosi cha timu hiyo.

Kikosi kina mchanganyiko wa nyota wanaocheza soka ndani na nje ya nchi wakiongozwa na nahodha Opa Clement anayeitumikia Eibar inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania.

Nyota wa timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20 ‘Tanzanite Queens’ ambao hivi karibuni wametoka kuitupa nje Angola katika mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia baadhi wamepata fursa ya kuwemo katika kikosi hicho cha Twiga Stars.

Kiungo ambaye amekuwa katika kiwango bora miezi ya hivi karibuni, Diana Lucas anayecheza soka la kulipwa Uturuki katika timu ya Trabzonspor ameendelea kuwemo katika kikosi hicho kinachojumuisha pia nyota wawili wanaocheza soka la kulipwa Mexico katika timu ya FC Juarez, Enekia Kasonga na Julitha Singano.

Wachezaji 25 wanaounda kikosi hicho ni Najat Abbas, Asha Mrisho, Donisia Misnja, Lidya Maximilian, Ester Maseke, Fumukazi Ally, Christer Bahera, Janeth Pangamwene, Elizabeth Chenge, Stumai Abdallah, Jamila Rajab na Winifrida Gerald wa JKT Tanzania.

Wengine ni Asha Ramadhan, Fatuma Issa na Aisha Mnunka wa Simba Queens, Enekia Kasonga na Julitha Singano (FC Juarez), Opa Clement (Eibar), Hasnath Ubamba (Al Masry), Noela Luhala (Asa Tel Aviv), Maimuna Kaimu (Yanga Princess), Nusrat Jaffar (Alliance Girls), Diana Lucas (Trabzonspor) na Suzan Adam (Tausi Queens).

Oktoba 22, 2025, Twiga Stars itakuwa nyumbani kuikabili Ethiopia na timu hizo zitarudiana jijini Addis Ababa, Ethiopia, Oktoba 28, 2025.

Mshindi wa jumla wa mechi mbili baina ya timu hizo, atafuzu Fainali za WAFCON 2026 zitakazofanyika Morocco mwakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *