Dar es Salaam. Serikali imekanusha uwepo wa vikundi vya uasi nchini kufuatia kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii zikionyesha watu wakijitambulisha kuwa wanahusika na harakati za vurugu katika baadhi ya mikoa.

Katika moja ya video iliyosambazwa kupitia Instagram, kijana anayejitambulisha kuwa mwanachama wa kikundi cha uasi alidai kuhusika na mauaji ya Mwenyekiti wa CCM Tawi la Itumbi, Elia Sambala, mkoani Mbeya, na kutishia kuendesha mashambulizi dhidi ya viongozi wa vijiji, kata na maofisa wa vyombo vya dola.

Hata hivyo, Februari 16, 2026, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilitoa taarifa kuwa Sambala aliuawa Februari 11, 2026 shambani kwake kwa kushambuliwa kwa kitu chenye ncha kali kichwani. Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, chanzo cha tukio hilo kilihusishwa na mgogoro wa masilahi katika eneo la uchimbaji dhahabu. Polisi walitangaza kuwashikilia watu wawili kuhusiana na mauaji hayo huku msako ukiendelea.

Video nyingine iliyosambaa katika mtandao wa X ilimuonyesha kijana mwingine akihamasisha kuundwa kwa vikundi vinavyodaiwa kusambaa Mbeya, Arusha na Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusu sakata hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema Serikali imefanya ufuatiliaji na kubaini kuwa hakuna kikundi chochote cha uasi kilichopo nchini. Amesema wanaoonekana katika video hizo ni Watanzania walioko nje ya nchi wanaojaribu kupotosha umma.

Ameongeza kuwa Serikali imelielekeza Jeshi la Polisi kufanya tathmini ya kina na kutoa taarifa rasmi kwa umma, huku hatua nyingine za kiusalama zikiendelea kuchukuliwa ndani ya vyombo husika.

Polisi yakazia

Mbali na kauli ya naibu waziri huyo, taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime, imekanusha maudhui ya video hizo, ikisema hakuna kikundi kilichoshiriki katika uhalifu wowote wa jinai.

“Jeshi la Polisi linakanusha taarifa wanazosambaza kuwa kikundi chao kimetenda uhalifu huu na ule kwani si za kweli,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Misime, leo Februari 22,2026.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jeshi hilo linawafuatilia kwa karibu watu hao, matamshi na jumbe zao wanazozitengeneza na kusambaza kwa lengo la kuleta taharuki kwa wananchi.

“Ufuatiliaji unafanywa usiku na mchana hivyo, wananchi muondoe hofu na endeleeni na shughuli zenu za kiuchumi na kijamii kama kawaida,” imeeleza taarifa hiyo.

Jeshi hilo, limewataka wananchi kuwapuuza watu hao, taarifa na jumbe zao, akisema hawapo nchini na hata wanachohamasisha hawatashiriki.

“Wananchi watambue lengo la watu hao ni kutaka kutuchonganisha, kutujengea chuki ili tuhamasike tujiingize kwenye uhalifu na vitendo vya vurugu,” imeandikwa katika taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesisitiza, Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua yeyote atakayeendelea kujihusisha na vitendo hivyo au kujiingiza katika uhalifu wa aina yoyote, kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *