Dar es Salaam. Mawakili wa mwanamuziki wa Hip-Hop nchini Marekani Sean “Diddy” Combs, wamekanusha taarifa zinazodai msanii huyo amempigia simu rais wa nchini hiyo Donald Trump akimuomba msamaha ili aweze kuachiwa huru baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi 50 jela.

Kwa mujibu wa timu ya wanasheria wa Diddy wametoa tamko hilo kupitia jarida la People wakieleza Diddy hajawahi kuomba msamaha wala msaada wowote kutoka kwa Trump. Hivyo taarifa hizo siyo za kweli huku wakidai zipuuzwe kwani zinapotosha umma.

“Hakuna mawasiliano rasmi yaliyofanyika kati ya Diddy na Rais Trump, wala timu yetu haijawasilisha ombi lolote la msamaha. Hivyo basi taaifa hizo zipuuzwe,” imeeleza taarifa hiyo. 

Aidha kwa mujibu wa ABC News, imeeleza Rais Trump wakati akizungumza na waandishi wa habari aliweka wazi kuwa watu wa karibu wa mwanamuziki huyo walimpigia simu na kumuomba msamaha.

“Nimepokea ujumbe wa moja kwa moja kutoka kwa watu wa karibu wa Diddy, wakiniomba nimtazame kwa huruma,” alisema Trump.

Aidha kwa upande wa wachambuzi wa masuala ya burudani nchini Marekani wanasema inawezekana kuna watu wa karibu wa Diddy walikuwa wakijaribu kumuombea msamaha rapa huyo bila idhini yake.

Kwa sasa, Diddy (Sean Combs) yupo katika gereza la Metropolitan Detention Center (MDC), Brooklyn, New York, ambapo atatumikia kifungo chake cha miaka 4 na miezi 2 (miezi 50). Hukumu ambayo imetolewa Oktoba 3,2025 baada ya kupatikana na hatia.

Mahakama ilimtaja kama mtu aliyekuwa akitumia umaarufu wake vibaya kuwanyanyasa kimwili na kisaikolojia baadhi ya wanawake waliokuwa wakifanya kazi au wakiishi naye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *