Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Movie, Wema Sepetu amekumbuka makubwa aliyofanyiwa na mashabiki wake mwaka 2022 ukiwamo upendo waliomwonyesha akiwa katika wakati mgumu na kukiri ameyaandika kwenye kitabu chake cha kumbukumbu.
Wema anasema moja kati ya mambo hayo ni kitendo cha mashabiki wake kuonyesha wako naye pamoja hata baada ya kushambuliwa na mfanyabiashara maarufu mitandaoni, Aristote aliyedai hana gari zuri la kifahari kama ilivyo kwa Irene Uwoya, kauli iliyopokelewa kwa hisia kali na wengi hadi Aristote mwenyewe kuomba radhi.

Akiongea na Mwananchi Wema ambaye aliwahi kuwa Miss Tanzania 2006, anasema kati ya vitu ambavyo hawezi kuvisahau kwa mashabiki zake, ni kitendo cha kuamua kumchangia pesa ili anunue gari ingawa hajawahi kuwaomba mchango. Pia amefunguka kuhusu sherehe yake ya siku ya kuzaliwa na jinsi nyota wa Yanga, Pacome Zouzoua anavyomchanganya kutokana na mavitu yake.
“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2022 na huwezi amini nimeandika kwenye kitabu changu cha kumbukumbu, mimi binafsi sikuwahi kumwambia mtu yeyote anichangie pesa. Nadhani ilikuwa ni upendo na watu wakaamua kuchanga, lakini niliwaambia siko tayari kukubaliana na hicho kitendo chao na wasitishe hilo zoezi na walisitisha. Sasa kwa kitendo hiki huwa nawathamini na kuwapenda sana mashabiki zangu, yaani huwa wanalia na mimi na kucheka na mimi ndiyo maana nawaheshimu sana.”

Sherehe ya ‘birthday’ bila mama
Anasema alifanya pati ndogo akiwaalika baadhi ya marafiki zake akiwamo mpenzi wake msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Whozu na kuhusu mama yake wao walishamalizana kwenye mambo hayo.
“Huwa sifuti kauli yangu, yaani nimekuwa tofauti na Wema wa zamani, akisema kitu hafanyi tena anakuja kukifanya. Septemba 28 ilikuwa birthday yangu, nikaita baadhi ya marafiki zangu akiwemo mpenzi wangu Whozu. Nia na madhumuni ilikuwa kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa na kuinjoi, ila haikuwa vile nilivyokuwa nafanyaga na hii ni kutokana na msimamo wangu niliousema sitafanya tena sherehe kubwa.”
“Kuhusu kama mama yangu nilimwalika, ipo hivi, mama sikumwalika kwa sababu nilimalizana naye kusheherekea nyumbani kama familia baada ya hapo ndiyo nikaenda kuungana na marafiki zangu, hivyo hakukuwa na tatizo lolote.”

Bifu na Lulu Diva
Kumekuwapo taarifa ya Wema na rafiki yake mkubwa Lulu Diva wameingia kwenye bifu na chanzo ni Lulu Diva kudaiwa kusababisha uhusiano wa Wema Sepetu na Whozu kuvunjika kama zilivyosambaa mtandaoni miezi michache iliyopita. Msikie mwenyewe;
“Niseme tu kwa sasa sina tofauti na Lulu Diva na ndiyo maana hata kwenye pati yangu ulimwona, ila ukweli kuwa na bifu na Lulu Diva, bifu hili huwa linanisumbua sana maana jinsi tulivyozoena kupiga stori kila wakati halafu itokee msizungumze kuna ugumu fulani hivi, lakini niliamini ipo siku tunaweza kumaliza tofauti zetu na huwa tuko hivyo na watu wasituingilie maana wataumbuka kwani kupishana ni jambo la kawaida na ugomvi wetu wala huwa haumhusu yeyote, ni sisi wenyewe tu na wakawaida.”

Pacome amvuruga
“Chaguo langu ni Pacome Zouzoua, wapo wachezaji wengi na wanacheza vizuri ila kwa huyu Pacome bado yuko kichwani mwangu. Siwezi taja majina ya timu yote sababu siwafuatilii sana, ila ukiniuliza mchezaji gani ananikosha akiwa uwanjani nitakwambia Pacome kwa sababu napenda anavyojituma uwanjani, yaani anapambana, pia anamuonekano mzuri hata akiwa nje ya uwanja, ukimuangalia tu, unasema yes! huyu ni bonge la mpambanaji.”

Usajili, jezi Yanga balaa
“Yanga imefanya usajili mzuri na kwa kuzingatia nafasi mbalimbali uwanjani, hivyo nawahurumia wapinzani watapata tabu sana. Msimu huu mambo yatakuwa moto Jangwani yaani tutapiga kila tutakayekutana naye, ukweli viongozi wamejitahidi nawapa pongezi.”
“Pamoja na kuongeza usajili wa Yanga, pia sitaacha kusifia jezi zao, ziko vizuri na kwa sisi mashabiki hazina pingamizi kwani chini unaweza kuvalia aina yoyote ya nguo na ukapendeza, nashangaa wanaoziponda.”