Simba Queens imetangulia fainali ya michuano ya Ngao ya Jamii kwa wanawake baada ya kuitandika Mashujaa Queens mabao 2-0 kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa KMC Complex Dar es Salaam.
Simba ambao ndio mabingwa wa kwanza wa kihistoria wanaandika rekodi nyingine ya kucheza fainali ya michuano hiyo mara pili sawa na mabingwa watetezi JKT Queens ambao wote wamechukua ubingwa mara moja.
Bao safi la Asha Omary dakika ya 33, liliivuruga Mashujaa ambayo ilionekana kucheza kwa kuzuia zaidi.
Hata hivyo, Simba iliendelea kushambulia lango la Mashujaa ambao waliendelea kuzuia na kushambulia kwa kushtukiza lakini kipa wa timu hiyo huku kipa Gelwa Yona akiokoa mipira ya hatari.
Hadi kipindi cha kwanza kinatamatika Simba ilikuwa mbele kwa bao moja, hata hivyo dakika ya 73 Aisha Mnunka alifanikiwa kuifungia timu yake bao la pili baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa JKT na kufunga bao safi la kideo hali ambayo ilimaliza matumaini ya Mashujaa.
Hata hivyo, timu zote zimeonyesha upungufu mkubwa, huku zikionekana kutokuwa na uelewano mzuri uwanjani.
Kikosi kilichoanza cha Simba, Zuhura Waziri, Ester Mayala, Ruth Ingosi, Zainah Nadende, Elizabeth Wambui, Asha Omary, Aisha Mnunka, Vivian Corazone, Jentrix Shikangwa, Cynthia Musungu na Z.Brice.
Kikosi cha Mashujaa, Gelwa Yona, Koku Kupanga, Sabina Mbuga, Patricia Salum, Zuhura Mlekwa, Zainabu Mohamed, Rehema Abdu, Veronica Mapunda, Tabea Aibano, Sharifa Hamidu, Veronica Gabriel.
Hii ni mara ya tatu michuano hiyo ichezwe kishirikisha timu zilizomaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, nusu fainali nyingine inayofuata itazikutanisha mabingwa watetezi JKT Queens na Yanga Princess.