
Iran, China, na Russia zimemuandikia barua ya pamoja mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya nyuklia (IAEA), kuthibitisha kumalizika kwa Azimio la Baraza la Usalama la UN 2231 pamoja na taarifa za shirika kuhusu mpango wa nishati ya nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika chapisho kwenye akaunti yake ya X Ijumaa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na Sheria na Masuala ya Kimataifa, Kazem Gharibabadi, amesema kuwa mabalozi na wawakilishi wa kudumu wa China, Iran na Russia wamemtumia barua Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi.
Amesema hatua hii imekuja kufuatia barua ya pamoja ya nchi hizi tatu kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama ikitangaza kumalizika kwa Azimio 2231 mnamo Oktoba 18.
Katika barua hiyo kwa mkuu wa IAEA, alibainisha, nchi tatu hizo zilithibitisha hatua “zisizo halali” zilizochukuliwa na nchi tatu za Ulaya — Uingereza, Ufaransa na Ujerumani — kutumia mfumo wa “snapback” wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran.
Iran imepinga hatua ya nchi hizo tatu za Ulaya ya kuanzisha mfumo wa snapback wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhdi yake na kutaka hatua hiyo kuwa “batili”.
Mnamo Oktoba 18, Tehran ilitangaza kumalizika kwa vikwazo vyote vya UN dhidi ya mpango wake wa nyuklia kufuatia kumalizika kwa Azimio la Baraza la Usalama la 2231.
Iran imekumbwa na mashinikizo endelevu ya kiuchumi katika miaka ya karibuni, hasa baada ya Marekani kujiondoa kwa upande mmoja kutoka katika makubaliano ya JCPOA mwaka 2018 na kurejesha vikwazo vikali chini ya sera iliyoitwa “mashinikizo ya juu kabisa.”
Licha ya changamoto hizo, Iran imejitahidi kujipanga upya kupitia kuimarisha uzalishaji wa ndani, kutumia mifumo ya biashara isiyotegemea dola ya Marekani, na kupanua uhusiano wa kiuchumi na washirika wake barani Asia, Afrika, Amerika ya Latini na mataifa jirani.