
Waziri wa Ulinzi wa Pakistan amesema, subira ya nchi yake kwa kundi la Taliban imemalizika na kwa hiyo imeingia kweye “vita vya wazi,” dhidi ya Afghanistan.
Khawaja Muhammad Asif ametangaza “vita vya wazi” dhidi ya serikali ya Taliban nchini Afghanistan kufuatia mapigano ya hivi karibuni ya mpakani kati ya vikosi vya majeshi ya nchi hizo mbili.
Katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa kijamii X, waziri wa ulinzi wa Pakistan amesema: “subira yetu imekwisha. Sasa ni vita vya wazi baina yetu sisi na nyinyi.”
Matamshi hayo makali yametolewa na Asif baada ya Taliban kudai kwamba vikosi vyao vimewaua wanajeshi kadhaa wa Pakistan na kuwakamata mateka wengine kadhaa katika operesheni ya mashambulizi ya mpakani.
Katka upande mwingine, Pakistan imefanya mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul na pia Kandahar, huku Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan Mohsin Naqvi akiyaelezea mashambulizi hayo kama “jibu mwafaka” kwa “uchokozi wa wazi wa Taliban.” Kituo kikubwa cha risasi katika jimbo la Nangarhar kimeripotiwa kuharibiwa, na mashambulizi dhidi ya maeneo mengine yangali yanaendelea.
Wakati huohuo, vituo vya kijeshi vya Taliban huko Kabul, Kandahar na Paktia navyo pia vimelengwa katika mashambulizi hayo. Duru za habari zimeripoti kuwa, ngome kadhaa za Taliban zimelengwa katika wilaya ya Kurram, na wapiganaji wanane wa kundi hilo wameuawa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa, hadi sasa wapiganaji wapatao 44 wa Taliban wameuawa katika operesheni hiyo ya mashambulizi.
Pakistan imetangaza kuwa, operesheni hiyo ni jibu kwa hatua zisizo na sababu zilizochukuliwa na Taliban ya Afghanistan katika eneo la mpakani, na kwamba mashambulizi ya anga yangali yanaendelea…/