New York, mji unaojivunia kuwa na tamaduni mbalimbali umekumbwa na wimbi la propaganda chafu na chuki dhidi ya Uislamu katika siku za mwisho za kampeni za uchaguzi wa meya wa mji huo, yaani tarehe 4 Novemba 2025.

Wimbi hilo limefika kileleni baada Zohran Mamdani, mgombea Mwislamu kutoka chama cha Democrat, kuongoza kuwatimulia kivumbi wagombea wenzake katika kura ya maoni na hivyo kuibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii ya Kiislamu ya mji huo.

Mamdani, ambaye ni msoshalisti wa kidemokrati mwenye asili ya Uganda na India, amekuwa akilengwa kwa mashambulizi ya maneno na propaganda za vyombo vya habari, kutokana na misimamo yake endelevu ya kutetea  makazi ya bei nafuu, usafiri wa bure wa umma na  ukosoaji wake wa sera za Israel. Mashambulizi hayo mara nyingi yamekuwa na mwelekeo wa propaganda chafu na chuki dhidi ya Uislamu. 

Chuki dhidi ya Uislamu zina rekodi ya muda mrefu huko New York lakini katika uchaguzi wa sasa, zimeshtadi kutokana na utambulisho wa kidini wa Mamdani na misimamo yake ya kisiasa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu huko New York (NYCIC), vitendo vya uhalifu vya chuki dhidi ya Waislamu vimeongezeka kwa asilimia 30 tangu Mamdani ashinde uchaguzi wa mchujo wa Wademokrati tarehe 24 mwezi Juni mwaka huu. Mabango ya kampeni ya Mamdani yameharibiwa katika vitongoji kama Queens na Brooklyn kwa kuandikwa maneno yenye kuudhi kama vile “gaidi” au “mfuasi wa sharia,” ambayo yanatokana na dhana na ufahamu potofu wa chuki ya Uislamu. Matukio haya si tu yamemweka Mamdani peke take chini ya mashinikizo, bali pia jamii nzima ya Waislamu na hivyo kumairisha hisi ya kutokuwa na amani miongoni mwa jamii hiyo. 

Mojawapo ya nukta muhimu katika uga ya sasa ni kauli zenye utata zilizotolewa na Meya wa sasa wa New York, Eric Adams, wakati alipotangaza kumuunga mkono hasimu wa kujitegemea wa Mamdani, Andrew Cuomo, Oktoba 23 mwaka huu. Adams, ambaye hapo awali aliunga mkono mashambulizi ya kibaguzi dhidi ya Mamdani, alisema katika hotuba yake kwamba: “New York inahitaji kiongozi ambaye anaunganisha jamii zote, na si yule anayehatarisha usalama wa jiji hili kwa misimamo ya mgawanyiko.” Japokuwa matamshi hayo hayakutaja  jina la Mamdani moja kwa moja, lakini yaliashiria misimamo yake kuhusu kupunguzwa bajeti ya polisi na kuikosoa Israel. Makundi ya kutetea haki za kiraia kama lile la CAIR-NY yameyahusisha matamshi hayo ya Eric Adams na chuki dhidi ya Uislamu” kwa sababu yalionekana kufungamanisha utambulisho wa kidini wa Mamdani na “suala la kuibua mgawanyiko.”

Eric Adams

Adams pia amemtaja Cuomo kama “kiongozi anayeaminika kulinusuru jiji hilo,” kitendo kilichotafsiriwa na wachambuzi wa mambo kama jaribio la kuwavutia wapiga kura wenye msimamo wa wastani na jumuiya za Kiyahudi, ambazo hazifurahishwi na misimamo ya Mamdani kuhusu Palestina.

Kauli na matamshi yote haya ni sehemu ya mkakati mpana zaidi wa wapinzani wa Mamdani ili kumuonyesha kama “mtu mwenye misimamo mikali”  au “asiye Mmarekani.”  Makundi ya kisiasa yaani PAC yanayomuunga mkono Cuomo, ikiwa ni pamoja na lile linaungwa mkono na meya wa zamani wa New York, Michael Bloomberg, ambalo lilitumia dola milioni 3.3 kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, yanamshambulia Mamdani na kutokana na hatua yake ya kuunga mkono harakati ya BDS, yaani harakati inayofanya kampeni ya kususia, kutofanya uwekezaji na kuiwekea vikwazo Israel. 

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Quinnipiac tarehe 9 mwezi huu wa Oktoba umeonyesha kuwa asilimia 41 ya wapiga kura Wayahudi wanamuunga mkono Cuomo; huku  Mamdani akiongoza kwa asilimia 62 kwa kuungwa mkono na wapiga kura raia wenye asili ya kigeni (hasa Waasia na Walatino). Mamdani na waungaji mkono wake akiwemo Alexandria Ocasio-Cortez na Bernie Sanders, wanachama wa harakati ya The Progressive Movement, wamelaani mashambulizi hayo na kuyataja kuwa jaribio lenye lengo la kupotosha masuala ya msingi kama vile mgogoro wa makazi na ukosefu wa usawa wa kiuchumi.

Zohran Mamdani alisema katika hotuba yake ya karibuni huko Bronx kwamba: “Mashambulizi haya hayahusu siasa, yanahusu utambulisho wangu. Mimi ni mwenyeji wa New York, na jiji hili ni letu sote.” Alisisitiza udharura wa kuwepo mazungumzo kati ya jamii zote na kuwataka wafuasi wake kutojibu misimamo ya chuki. 

Mazingira haya ya propaganda chafu na chuki dhidi ya Uislamu, licha ya kuathiri uchaguzi, ni kengele ya hatari kwa mustakbali wa sera ya kuishi pamoja kwa maelewano huko New York. Jumuiya za kiraia zimetoa wito wa kufuatiliwa ipasavyo vitendo vya uhalifu wa chuki na kutaka kufanyike kampeni za utoaji elimu. Kutokana na kukaribia siku ya uchaguzi wa meya wa mji wa New York, swali hili linaulizwa kwamba, je wakazi wa mji huo wataheshimu sera ya kuishi pamoja kwa amani watu wa mbari na tamaduni tofauti au watasalimu amri mbele ya hofu na mgawanyiko ulioibuliwa na Muungano wa Wahafidhina na wale wanaopinga Uislamu?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *