Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na Khalifa Haftar na ambalo linadhibiti eneo la mashariki mwa Libya, lilitangaza jana Ijumaa kwamba limefanikiwa kukomboa raia kadhaa wa Niger waliokuwa wametekwa nyara na kundi moja lenye silaha la Niger tangu miezi 16 iliyopita.

Katika taarifa yake kiliyoitoa kwenye ukurasa wake wa Facebook, Kitengo cha Habari za Vita cha Jeshi la Taifa la Libya (LNA) kimesema kuwa, operesheni maalumu imefanywa kuwaokoa raia hao wa Niger waliotekwa nyara na kundi haramu lenye silaha karibu na Al-Qatrun kusini magharibi mwa Libya. Eneo hilo liko umbali wa takriban kilomita 180 kutoka mpaka wa Libya na Niger.

Taarifa hiyo haikutaja idadi kamili ya watu hao waliokombolewa, lakini video iliyoambatanishwa na taarifa hiyo inaonesha watu watano wakishuka kutoka kwenye ndege ya kijeshi ya LNA. Katika picha hiyo, mmoja wa mateka waliokombolewa anasikika akisema kwamba walikuwa wametekwa nyara na kundi la waasi la Niger linalojiita Patriotic Front for Justice (FPJ). Hilo ni kundi haramu lenye silaha ambalo linaendesha uhalifu wake nchini Niger. Mateka huyo aliyekombolewa anasikika pia akisema kwamba walitekwa nyara tarehe 21 Juni mwaka jana 2024. 

FPJ ni kundi la waasi nchini Niger linalopinga baraza tawala la kijeshi. Baraza la Kijeshi liliundwa nchini Niger baada ya kuchukua madaraka kufuatia mapinduzi ya 2023 yaliyomng’oa madarakani Rais Mohamed Bazoum ambaye wananchi wa Niger walikuwa wanamlalamikia vikali kwa kuwa kibaraka mkubwa wa dola la kikoloni la Ufaransa na ambaye alikuwa hajali kabisa maslahi ya nchi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *