Dar es Salaam. Baada ya ukimya wa muda mrefu, msanii wa Bongofleva, 20 Percent ameibuka na kusema hajarogwa kama baadhi ya watu wanavyodai na amewataka mashabiki kuacha mambo ya uzushi.
20 Percent ambaye aliwahi kuteka nyoyo za mashabiki wengi kupitia nyimbo zenye ujumbe mzito wa kijamii, ameliambia Mwananchi kuwa ukimya wake umetokana na ubize wa majukumu mengine hivyo sasa amerudi rasmi kwenye anga la muziki na kuachia wimbo unaoitwa ‘Ni Upendo’ pamoja na video yake.
“Kwasasa nimeamua kurudi kwenye muziki, nimeachia wimbo wangu unaoitwa ‘Ni Upendo’ na video yake pia, maana nimeona mashabiki wangu wamekuwa wakiniulizia sana kama nimeacha muziki au vipi, na wapo ambao wanasema nimerogwa ndio maana nipo kimya, ila ukweli sijarogwa na huwa siamini imani za kishirikina mimi, kukaa kwangu kimya ni majukumu tu ya hapa na pale yamenizidi.”
20 Percent aliwahi kutikisa na nyimbo kama ‘Binti Kimanzi’, ‘Mama Neema’, ‘Tamaa Mbaya’, na nyingine nyingi ambazo zilihamasisha, kuelimisha na kuibua mjadala katika jamii kuhusu maisha ya kila siku.