
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mathew Mwaimu ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa za kupiga kura kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Pia, ametoa wito kwa wadau wote wa uchaguzi vikiwemo vyombo vya usalama, waandishi wa habari na vyama vya siasa, kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na kuheshimiana ili kutoa fursa sawa kwa kila mwenye sifa kutumia haki yake ya kikatiba.
Kwa mujibu wa tamko la THBUB lililotolewa leo Oktoba 27, 2026 kwa umma, kuhusu ushiriki wa wananchi katika uchaguzi mkuu huo, Mwaimu amesema kuwa kushiriki uchaguzi ni haki ya kikatiba inayomwezesha kila Mtanzania kuchagua viongozi wanaowataka kwa kipindi cha miaka mitano kama inavyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Amesema wananchi wote waliotimiza umri wa miaka 18 na waliojiandikisha na kupata vitambulisho vya kupigia kura, wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kikatiba kwa kujitokeza kupiga kura ili kuhakikisha demokrasia inaimarika na sauti za Watanzania zinasikika kupitia sanduku la kura.
Katika kuelekea uchaguzi huo, amesema THBUB imeendesha mafunzo kwa askari wa Jeshi la Polisi na waandishi wa habari katika mikoa 14 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar kwa lengo la kuwakumbusha umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu, na misingi ya utawala bora wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Amesema Tume hiyo inaendelea kufuatilia kampeni za uchaguzi zinazoendelea kufanywa na vyama mbalimbali vya siasa ili kuhakikisha zinazingatia haki, usawa na sheria za nchi.
Mwaimu kupitia tamko hilo amesisitiza kuwa haki ya kupiga kura ni nyenzo muhimu ya wananchi kushiriki katika utawala wa nchi na kuchagua viongozi wanaowaamini, akiongeza kuwa kila kura ina mchango mkubwa katika kuamua mustakabali wa Taifa.
“Nichukue fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kutumia haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kupiga kura ili kuchagua viongozi katika ngazi ya Rais, ubunge na udiwani,” amesema Mwaimu.
Katika uchaguzi huo unaoshirikisha vyama vya siasa 18, vilivyopata usajili wa kudumu ikiwemo chama tawala cha CCM, kampeni zake zinatarajiwa kufungwa rasmi kesho baada ya miezi miwili kuwafuata wananchi kunadi sera zao kushawishi umma kuwapigia kura ya kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Jumla ya Watanzania milioni 37.6 ndiyo wenye dhamana ya kuamua nani awe diwani, mbunge au Rais kwa kipindi cha miaka mitano ijayo hadi 2030 na kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jumla ya vituo vya kupigia kura ni 99,895.
Katika mgawanyo huo, Tanzania Bara itakuwa na vituo 97,348 na Zanzibar wanaoanza kesho kupiga kura ya mapema watakuwa na vituo 2,547 ambavyo Watanzania waliokidhi sifa watatumia kumchagua kiongozi wamtakaye.