Mwanza. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema utendaji bora wa mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan umewafunga midomo na kufifisha ndoto za baadhi ya watu waliotaka kumuhujumu na kuiparaganyisha Serikali.

Kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoachiwa na mtangulizi wake wa urais, hayati John Magufuli ikiwemo Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), Daraja la Kigongo Busisi na miradi mingine mikubwa ya kimkakati, amani na mshikamano wa Taifa unatajwa kumfanya kuwa kivutio cha Watanzania wengi.

Samia, aliyekuwa Makamu wa Rais aliingia madarakani Machi 19, 2021, siku mbili kupita baada ya Rais Magufuli kufariki dunia. Samia akaapishwa kuendelea na muhula wa pili aliokuwa ameuanza Magufuli.

Baada ya kuapishwa, Rais Samia alisema ataiendeleza miradi mbalimbali iliyokuwa imeanzishwa na mtangulizi wake na kuanzisha mipya. Miradi hiyo ameikamilisha yote.

Leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tathimini ya mikutano ya kampeni ya Samia amesema kazi kubwa imefanyika chini ya Rais huyo.

Kampeni za uchaguzi mkuu ulioanza Agosti 28 zitahitimishwa kesho Jumanne, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo tayari Samia amefanya mikutano 114 nchi nzima ikiwemo Zanzibar na keshokutwa Jumatano ya Oktoba 29, 2025 itakuwa siku ya upigaji kura.

Kihongosi amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia ameonyesha uwezo wake wa kusimamia miradi mbalimbali ikiwemo ya kimkakati na kuwa uwezo wake wa utendaji kazi umewatetemesha na kufifisha ndoto za waliokuwa wanataka urais na kutaka kuipasua Serikali.

“Miaka minne ya Samia nani alijua daraja la Mwalimu Nyerere litaisha, nani alijua SGR itaisha, Daraja la Kgongo-Busisi. Uwezo wake umewatingisha na kuwatetemesha. Waliamini atafeli wameona chombo kimetulia na kimesonga mbele. Oktoba 29, 2025 tunaenda kushinda kwa kishindo kuliko wakati wowote Mungu tunayemwamini na Mungu tunayeishi anaenda kutuheshimisha,” amesema Kihongosi.

“Kuna watu (bila kuwataja) walikuwa na ndoto za urais, zimeyeyuka baada ya kuona mama anachapa kazi kuliko maelezo, sasa wanamchafua, tushikamane, tulinde nchi yetu, tumlinde Rais na Taifa letu. Vijana sisi ndio walinzi wa kwanza wa Taifa hili hatukubali kama vijana wa Kitanzania mtu yoyote aharibu taifa letu ambalo limetulea tusipolinda nchi hii hatuna pa kwenda,” amesema.

Kihongosi amesema:”Kuna watu walitaka hiki chama kiharibike wamekwama, kuna watu walitaka Serikali ipasuke wamekwama, wanaleta nongwa. Wanataka kuitisha mamlaka, kuitisha nchi, kuitisha Serikali ionekane mambo hayako sawa, nawahakikishia Tanzania hii chini ya Samia ni salama sana na Mungu aliyempa uongozi ndiye atakayemlinda na kumvusha sisi Wakristo tunaamini hivyo.”

Kihongosi amewataka Watanzania kutambua wanaowashawishi wafanye vurugu wana hati za kusafiri, wana marafiki nchi za nje na kuwa pakiharibika nchini hakuna pa kukimbilia.

“Niwaambie hapa kulikuwa na viongozi waliokuwa na matamanio fulani fulani yamekwama, tumekaa kimya kwa muda mrefu tumewapuuza kwa muda mrefu lakini wanachokoachokoa, sasa niwaambie wale walikuwa na ajenda zao za kupasuka chama za kupasua Serikali lakini wamefanya nini wamegota. Niwaambie chama hiki hakitingishwi, CCM haitikisiki, CCM ni imara na madhubuti,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *