Dar es Salaam. Msanii wa R&B na Bongo Flava, Khery Sameer Rajab ‘Mr Blue’ ameelezea namna anavyofanya kazi zake kwa umakini, kuhakikisha zinaishi kwa muda mrefu.

Amesema licha ya kumiliki studio, ni ngumu kuingia mara kwa mara na kurekodi kwa mazoea, badala yake anatumia muda mwingi kwa mwendo wa kinyonga, kuumiza akili kuandika nyimbo ambazo zinaleta maana kwa jamii.

“Msanii akiwa na studio anaweza akawa anafanya mazoea na kazi, mfano wimbo ambao unataka ukae kwa muda mrefu masikioni mwa mashabiki ambao wajionea ni sehemu ya maisha yao, huwezi kuingia studio siku moja na kuumaliza,” amesema Mr Blue na kuongeza;

“Mfano wimbo wangu wa Tabasamu niliuandika takribani mwaka mmoja na nusu, nikipanda jukwaani bado watu wanavaibu nao (licha ya kwamba una zaidi ya miaka 16 tangu ulipotoka 2009), kwani mashairi yake yanaishi.

“Ukiwasikiliza wasanii wakubwa duniani projekti zao wanazifanya kwa muda mrefu, ndio maana nyimbo zilizoimbwa miaka mingi bado zinagusa mashabiki na zinapendwa.”

Amesema anapoandaa wimbo ana prosesi anazozizingatia ya kwanza ni kuuandika, jambo la pili anauvundika nakuuharibu tena ili kupanua mawazo (idea), halafu kuufanyia mazoezi, kisha kwenda studio kurekodi.

“Nikienda kurekodi hadi prodyuza anafurahia ninachokifanya, maana sichukui muda wake mwingi kurudiarudia kuimba, hilo ndilo linanifanya nisiwe nakurupuka mara kwa mara kwenda studio kurekodi,” amesema Mr Blue ambaye nje na muziki anapenda mchezo wa ngumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *