
Mwandishi wa habari raia wa Uingereza anayejulikana kwa kuunga mkono Palestina amekamatwa nchini Marekani na shirika la Uhamiaji na Forodha (ICE), kufuatia shinikizo kutoka kwa makundi yanayoiunga mkono Israel.
Sami Hamdi, mchambuzi wa siasa na mwandishi mashuhuri, alikamatwa na maafisa wa ICE katika uwanja wa ndege wa San Francisco siku ya Jumapili.
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) lililaani kukamatwa kwake likitaja tukio hilo kuwa “hujuma ya wazi dhidi ya uhuru wa kujieleza,” na kulihusisha na ukosoaji wake wa wazi dhidi ya vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na Israel dhidi ya Gaza.
Hamdi, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa sera za Marekani na Israel, alikuwa amehutubia hafla ya CAIR huko Sacramento Jumamosi usiku, na alitarajiwa kuhutubia hafla nyingine ya CAIR huko Florida siku iliyofuata kabla ya kuzuiliwa.
CAIR ilieleza kuwa kukamatwa kwa Hamdi kulifuatia kampeni ya pamoja ya “mrengo wa kulia wenye misimamo mikali, wenye sera za ‘Israel Kwanza’,” ikitangaza kuwa, “Taifa letu lazima likomeshe utekaji wa wakosoaji wa [utawala wa Israel] kwa amri ya watu wenye misimamo mikali wa ‘Israel Kwanza’ … Hii ni sera ya ‘Israel Kwanza’, siyo ya ‘Marekani Kwanza’, na lazima ikome.”
Mwanaharakati wa mrengo wa kulia Laura Loomer, mshirika wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye hujifaharisha kwa misimamo yake ya chuki dhidi ya Waislamu huku akijiita “mtetezi wa wazungu,” alijigamba mtandaoni kuhusu mchango wake katika tukio hilo.
Loomer alimwambia Hamdi, “Una bahati kuwa adhabu yako ni kukamatwa na kufukuzwa tu,” akimtaja kuwa “mfuasi wa Hamas na Ikhwanul Muslimin.”
Loomer na wengine walihusisha hatua dhidi ya Hamdi na taasisi ya RAIR (Rise Align Ignite Reclaim), kundi la shinikizo linaloiunga mkono Israel ambalo linadai kupambana na kile wanachokiita “ubabe wa Kiislamu.”
Taasisi hiyo hivi karibuni ilidai, bila ushahidi, kuwa Hamdi alikusudia “kueneza mtandao wa kisiasa wa kigeni unaopinga maslahi ya Marekani,” na hivyo kuhimiza serikali imfukuze.
Wafuasi na watetezi wa haki za kiraia wanasema kukamatwa kwa Hamdi ni mfano mwingine wa kisasi cha kisiasa dhidi ya wakosoaji wa Israel, wanaoadhibiwa mipakani hata kabla ya kupewa jukwaa la kuzungumza.
Tangu Israel ianze mashambulizi yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, takriban Wapalestina 68,000 wameuawa na wengine 170,000 kujeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Wataalamu wanaonya kuwa idadi halisi ya vifo huenda ikafikia mamia ya maelfu pindi waliopotea au waliokwama chini ya vifusi watakapohesabiwa.