Moshi. Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, amesema kuwa endapo atapata ridhaa ya wananchi kuwakilisha bungeni, atahakikisha vijana wanaofanya kazi ya bodaboda na bajaji kwa mikataba ya kila siku wanapata mfumo bora utakaopunguza mzigo wa marejesho.

Shayo amesema kwa sasa vijana wengi wanaofanya kazi hizo hulazimika kurejesha hadi Sh10,000 kwa siku kwa wamiliki wa vyombo hivyo, hali inayowafanya washindwe kujikwamua kiuchumi.

Akizingumza  leo Oktoba 27 wakati akifunga mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya stendi ndogo ya mabasi mjini Moshi, amesema kupitia sera na mikakati yake, atahakikisha mfumo mpya unaowezesha vijana kurejesha kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000 kwa siku unaanzishwa, ili kuwawezesha kupata kipato kinachowainua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

“Vijana wa bodaboda na bajaji najua shida zenu, Nawaahidi zitakwisha, mtakapokwenda kunichagua Oktoba 29 nataka niwahakikishie ile mikataba mnayopewa na matajiri ya kuwafunga, kwangu itakuwa ni historia,”amesema Shayo

Amesema”Nakwenda kutengeneza mfumo wa kuwapa bajaji na bodaboda kwa riba kidogo ambayo itawasaidia nyie badala ya kurejesha Sh10,000 mnarejesha Sh2000 hadi Sh3000 na maisha yanakwenda.”

Aidha, amewaomba wananchi wa Jimbo hilo kuhakikisha Oktoba 29, wanajitokeza kwenda kupiga kura na kumchagua Rais anayetokana na chama hicho, Samia Suluhu Hassan na yeye kuwa Mbunge wa Jimbo hilo ili wananchi wa Jimbo hilo waendelee kunufaika na serikali ya chama hicho kwa kupata miradi mingi ya maendeleo.

“Nawaahidi wana Moshi mjini sitawaangusha. Kuna mambo mengi ya kufanya hapa, naomba nafasi hii ili niweze kuwatumikia ninyi, tuna kila sababu ya kwenda kumpa kura Rais wetu, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa chini ya serikali yake amefanya mambo makubwa katika Jimbo hili hususani kwenye miradi ya afya, maji, elimu, barabara pamoja na mambo menu mazuri ambayo ameyafanya,”amesema Shayo

Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye akizungumza wakati wa ufungaji wa kampeni katika Jimbo la Moshi mjini.Picha na Janeth Joseph

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye amemwombea kura mgombea Urais wa Chama hicho, Samia Suluhu Hassan akisema amefanya mambo makubwa katika Kanda ya Kaskazini na kuwaomba wananchi kujitokeza Oktoba 29 kumpa kura za kutosha.

“Niwaombe watu wote wa Jimbo hili waliojiandikisha kwenda kupiga kura Oktoba 29 na kumpa Rais Samia Suluhu Hassan kura za kutosha, natamani Jimbo hili liongeze kwa kumpa kura za kutosha kwani amefanya mambo makubwa na mazuri ya kuridhisha katika mkoa huo,”amesema Sumaye

Kwa upande wake, mjumbe wa kamati ya siasa wa CCM  mkoa wa Kilimanjaro, Adam  Besti Simba amewaomba wananchi wa Jimbo hilo kujitokeza kwa wingi siku ya Oktoba 29 na kwenda kumpigia kura za kutosha mgombea Urais wa Chama hicho Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo, Ibrahim Shayo ili wazidi kuleta maendeleo katika Jimbo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *