Ally Salim Ngwando siyo jina dogo licha ya mwenye jina kuwa na umbo dogo akiwa na uzito wa kilo 51 katika mchezo wa ngumi za kulipwa.

Mitaa ya Manzese ndiyo imemlea bondia huyo wa ngumi za kulipwa mwenye miaka 26 akiwa na rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 15 sawa na raundi 83. Licha ya sasa kupanda ulingoni na kucheza ngumi, lakini mwenyewe anasema zamani alikuwa mwanasoka, lakini mazingira yakamfanya avue njumu na kuvaa glavu hadi sasa.

Ngwando kwa mujibu wa rekodi yake siyo bondia mzuri wa kushinda kwa knockout kwani amefanikiwa kushinda 11 kati ya hayo mapambano mawili pekee ameshinda kwa knockout tena kwa asilimia 18.18.

Lakini kwa upande wa kupoteza, amepigwa mara mbili kati ya hizo moja ni knockout na ametoka sare mara mbili.

Katika uzani wa fly, Ngwando anakamata nafasi ya saba katika mabondia 33 wa uzani huo wakati duniani akiwa wa 173 katika mabondia 786 huku akiwa amepewa hadhi ya nyota moja na nusu.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na bondia huyo aliyeanza kupanda ulingoni kwenye ngumi za kulipwa mwaka 2016 ambapo tumetaka kufahamu nini kinachomkwamisha kimafanikio licha ya rekodi yake kuwa kubwa, lakini pia namna alivyoingia katika mchezo huo.

Ngwando anafafanua kuwa sehemu kubwa ya kukwama kwake ni kukosa nafasi ya kuonekana ndiyo maana amekuwa akikaa kwa muda mrefu pasipo kupanda ulingoni.

“Siwezi sema kwamba sipendi hapana lakini sababu kubwa imetokana na kukosa nafasi ya kuweza kupigana.

“Nadhani mapromota hawatuoni pengine lakini siyo suala la kufanyiwa hujuma ingawa naamini wakati ukifika wa Ngwando kuonekana kwenye ulingo basi kila mmoja ataniona.

“Kitu pekee kikubwa ni kuendelea na mazoezi na kujiweka sawa japo kuwa ni jambo ambalo linakuwa linaumiza  kwa kutopata nafasi ili watu waone mafanikio yangu.

Kitu gani kilifanya upende mchezo wa ngumi?

“Kitu ambacho kilinifanya niingie kwenye ngumi ni kwa sababu niliupenda mchezo wa ngumi ingawa mimi ni mpenzi wana wa mchezo wa soka kwa sababu nilicheza huko nyuma.

“Unajua nilipenda ngumi kwa sababu ya mitaa niliyotoka, Manzese ni jambo la lazima kama mtu hajawa mcheza mpira basi atakuwa bondia.

“Nilikuwa nacheza mpira lakini nilikuwa naona watu wakifanya mazoezi ngumi, nikavutiwa nao, nikaanza kufanya mazoezi na nilichotegemea, kimeenda kunilipa kwenye ngumi.

“Nilitamani kuwa mtu mkubwa sana endapo nitacheza mpira, lakini Mungu amenijalia kwenye ngumi ndiyo kama hivi

Kitu gani kikubwa umekipata kwenye ngumi?

“Binafsi nadhani cha kwanza ni umaarufu lakini kitu cha pili kupata ridhiki, napata kwa sababu ya ngumi, ukiachana na kucheza lakini kuna watu wanajua kazi yangu, inakuwa rahisi nikikutana nao  kupata kunisaidia.

Umewahi kulipwa pesa nyingi, kiasi gani kwenye ngumi?

“Pesa nyingi ambayo niliwahi kulipwa, nilisafiri kwenda Namibia, nilipata milioni nne na vichenji kadhaa ambazo nilitu-mia kununulia kiwanja.

Uwezo wako wa kula ni kiasi gani?

“Siwezi kusema uwezo wangu wa chakula, nakula vipi, hivi ni kwa sababu hatuna pesa lakini nyumbani kwa bondia vyakula havitakiwi kukauka ambavyo vyote vinakuwa msaada wa kukupa utulivu na nguvu wakati wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *