Dar es Salaam. Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC) na Jukwaa la Mabunge la Mkutano wa Kimataifa wa Kanda ya Maziwa Makuu (FP-ICGLR) wamesaini makubaliano ya ushirikiano (MoU) yenye lengo la kufikia afya bora, utawala imara, diplomasia na ushirikiano wa kina wa kikanda.

Ushirikiano huo utaanzisha Kituo cha Umahiri cha Kikanda cha Diplomasia na Utawala wa Afya, kitakachokuwa kitovu cha mafunzo kwa wabunge, maofisa wa Serikali na wataalamu wa kiufundi katika maeneo ya mazungumzo ya kidiplomasia, uundaji wa sera na ushirikiano wa kuvuka mipaka.

Pia, kitakuwa taasisi ya tafiti za kimkakati, kikizalisha ushahidi wa kuunganisha afya ndani ya mifumo mipana ya amani, usalama na maendeleo.

Makubaliano hayo, yaliyosainiwa jana Jumapili Oktoba 26, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, Dk Ntuli Kapologwe na Katibu Mkuu wa FP-ICGLR, Dk Deo Mwapinga, yanaonyesha dhamira inayoongezeka kati ya taasisi za kiserikali na za kibunge kushirikiana katika kukabiliana na changamoto za pamoja za afya na maendeleo.

Kupitia ushirikiano huu, taasisi hizo mbili zitashirikiana katika maeneo muhimu kama vile ujenzi wa uwezo wa wabunge, uimara wa mifumo ya afya, uoanishaji wa sera, ujumuishaji wa wanawake na vijana, utawala wa kidijitali wa afya, pamoja na kukuza demokrasia na haki ya kupata afya bora.

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo, Dk Kapologwe amesema watu wenye afya njema ndio msingi wa mataifa yenye amani na ustawi.

“Ushirikiano huu unatupatia nafasi ya kuunganisha wadau wa afya na utawala ili kutengeneza sheria, sera, na uwekezaji unaotokana na ushahidi wa kisayansi kwa manufaa ya mamilioni ya watu katika kanda hii,” amesema.

Amesisitiza magonjwa hayana mipaka. Kuanzia milipuko ya magonjwa hadi usugu wa vimelea vya maradhi, kutoka changamoto za afya ya mama na mtoto hadi ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, hizi zote ni changamoto za kikanda zinazohitaji suluhisho la kikanda.

“Ili kukabiliana nazo ipasavyo, lazima tuende zaidi ya juhudi za kila nchi peke yake na tushirikiane kujenga mifumo ya afya iliyopangwa, endelevu na yenye usawa. Pia tunapozidi kuimarisha mifumo yetu ya afya, ni lazima pia tutambue kwamba baadhi ya hatua muhimu zaidi, ikiwemo sheria na mifumo ya sera zinahitaji sauti ya wananchi ili ziweze kupitishwa kisheria,” amesema.

Dk Kapologwe amesema kupitia makubaliano hayo, ECSA-HC itatumia uongozi na ushawishi wa wabunge kutoka kote Ukanda wa Maziwa Makuu kuhakikisha kwamba wanatekeleza wajibu wao muhimu wa usimamizi.

“Pamoja watahimiza uoanifu wa sera, kuhamasisha dhamira ya kisiasa, na kutoa uungwaji mkono wa kisiasa unaohitajika kutafsiri ahadi za afya kuwa vitendo vya kudumu,” amesema.

Pia ametaja nguzo muhimu ya ushirikiano huo ni kuanzishwa kwa Kituo cha Kikanda cha Umahiri katika Diplomasia na Utawala wa Afya, ambapo wabunge, maafisa wa serikali, na wataalamu wa kiufundi watafundishwa na kupewa uwezo wa kushiriki katika uundaji wa sera za juu, majadiliano, na ushirikiano wa kuvuka mipaka.

Kituo hiki pia kitakuwa ni jukwaa la tafiti na mawazo, likizalisha na kutafsiri ushahidi kuwa sera zinazoweza kutekelezeka ambazo zinaunganisha afya na mifumo mikubwa ya amani, usalama na maendeleo.

Kwa upande wake, Dk Mwapinga, amesisitiza umuhimu wa uongozi wa kibunge katika kubadilisha matokeo ya afya;

“Mabunge yana jukumu muhimu katika kuhakikisha uwajibikaji na uendelevu wa ahadi za afya. Kupitia makubaliano haya, tunalenga kuwawezesha wabunge kwa zana na maarifa yatakayowawezesha kuhimiza sera za afya jumuishi na zenye tija,” amesema.

Amesema kupitia ushirikiano huo, wanalenga kujenga daraja kati ya watunga sera na watekelezaji, kuhakikisha kwamba sheria, bajeti, na majukumu ya usimamizi yanaakisi kwa uhalisia mahitaji ya jamii na kujibu ipasavyo changamoto mpya za kiafya.

“Tutashirikiana pia katika kuanzisha Kituo cha Kikanda cha Umahiri katika Diplomasia na Utawala wa Afya mpango ambao utaimarisha uwezo wetu wa kushiriki katika majadiliano, utungaji sera unaotegemea ushahidi, na ushirikiano wa mipakani.

“Kituo hiki kitakuwa kitovu cha kikanda cha kubadilishana maarifa, kikiwawezesha wabunge na wataalamu wa afya kuwa mabalozi wa maono ya maendeleo yanayoweka afya na utu wa binadamu katikati,” amesema.

Balozi Mwapinga amesema Jukwaa la Mabunge, liko tayari kuunga mkono utekelezaji kamili wa makubaliano hayo kupitia Timu ya Pamoja ya Utekelezaji wa Mradi, itakayohakikisha uratibu, uhamasishaji wa rasilimali, na uwajibikaji.

“Ninaziomba serikali zetu, wafadhili, na asasi za kiraia kushirikiana nasi katika kuunga mkono mpango huu. Mustakabali tunaoutamani utapatikana tu tukifanya kazi kwa pamoja,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *