BAADA ya Azam na Singida Black Stars kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, zina kibarua cha kukutana na vigogo.

Timu hizo zinashiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza ambapo kwa mujibu w Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), zitakuwa chungu (POT) namba nne wakati wa upangaji wa makundi na ratiba ya hatua hiyo.

Azam FC na Singida Black Stars zote zikiwa katika POT 4, jambo linalomaanisha hazitakutana hatua ya makundi, lakini vigogo waliopo POT 1, 2 na 3, watakuwa mikononi mwao.

Timu zingine zilizopo Pot 4 ni Olympic Safi (Morocco), Zesco United (Zambia), San Pedro (Ivory Coast) na Nairobi United (Kenya).

POT 1 ina timu vigogo ambazo ni Zamalek SC (Misri), Wydad Athletic Club (Morocco), USM Alger (Algeria), na CR Belouizdad (Algeria).

POT 2 zipo Stellenbosch FC (Afrika Kusini), Al Masry (Misri), Maniema Union (DR Congo), na Djoliba AC (Mali). Wakati POT 3 ni Kaizer Chiefs (Afrika Kusini) na AS Otoho (Congo Brazzaville).

Kwa mpangilio huu, Azam FC na Singida Black Stars zinakabiliwa na changamoto ngumu katika makundi yao, lakini kutokana na matokeo mazuri ya hivi karibuni, kuna matumaini kwamba klabu za Tanzania zitaendelea kufanya vizuri na kuendeleza heshima ya soka la nchi kimataifa.

Mashabiki wa soka nchini wanasubiri kwa hamu droo hiyo ya CAF iliyopangwa kufanyika Novemba 3, 2025 jijini Johanesburg nchini Afrika Kusini ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania itakuwa na timu nne hatua ya makundi. Kumbuka Ligi ya Mabingwa zipo Yanga na Simba.

ZILIZOFUZU MAKUNDI SHIRIKISHO
Zamalek SC (Misri)
Wydad AC (Morocco)
CR Belouizdad (Algeria)
USM Alger (Algeria)
Al Masry (Misri)
Stellenbosch FC (Afrika Kusini)
Djoliba (Mali)
AS Maniema (DR Congo)
Kaizer Chiefs (Afrika Kusini)
Otoho d’Oyo (Congo)
Azam FC (Tanzania)
ZESCO United (Zambia)
San Pedro (Ivory Coast)
Singida Black Stars (Tanzania)
Olympique de Safi (Morocco)
Nairobi United (Kenya)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *