Rombo. Zikiwa zimepita siku 22 tangu bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Mkuu, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro kuteketea kwa moto, bweni jingine la shule hiyo lenye wanafunzi 160 limeteketea tena kwa moto usiku wa kuamkia leo Jumanne, Oktoba 28, 2025.

Tukio la kwanza lilitokea Oktoba 6, 2025, ambapo bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 90, linalomilikiwa na Kanisa Katoliki wilayani humo, liliteketea kwa moto wakati wanafunzi wakiwa kwenye ibada ya asubuhi.

Katika tukio hilo, mali zote za wanafunzi ziliteketea kwa moto ikiwemo magodoro 91, vitanda 46, nguo, madaftari na vifaa vingine vya matumizi binafsi.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema tukio hilo limetokea usiku wa Oktoba 27 na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali, ingawa hakuna majeruhi wala vifo vilivyoripotiwa.

“Tulipokea taarifa za moto katika bweni la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mkuu lililopo Kata ya Makiidi, Wilaya ya Rombo, tulifika haraka eneo la tukio na kukuta moto ukiendelea kuwaka ndani ya bweni, Askari wetu walifanya jitihada na kufanikiwa kuuzima moto huo kabla haujasambaa zaidi,” amesema Kamanda Mkomagi.

Kamanda Mkomagi amesema chanzo cha moto huo bado hakijabainika na uchunguzi unaendelea ili kubaini sababu hasa ya matukio hayo ya moto katika shule hiyo.

“Katika tukio hili hakuna aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa, lakini vitanda 89, magodoro 160, ofisi moja pamoja na madaftari ya wanafunzi vimeteketea kwa moto,” amesema Kamanda Mkomagi.

Aidha, Kamanda Mkomagi ametoa wito kwa wananchi, taasisi za elimu na jamii kwa ujumla kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto, na kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia namba ya dharura 114 pindi wanapobaini hatari ya moto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *