Kuzimwa kwa huduma za mawasiliano nchini Afghanistan mwezi Septemba 2025 kumeathiri vibaya maisha ya watu, kwa mujibu wa ripoti  iliochapishwa leo na  Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR)  na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan (UNAMA).

Msemaji wa OHCHR, Jeremy Laurence, akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi hii leo ametaja madhara hayo kuwa ni  “Kuanzia mifumo ya afya hadi sekta ya benki na shughuli za kila siku za biashara ndogo, watu wa Afghanistan wanategemea sana mifumo ya mawasiliano kupata huduma muhimu.”

Ripoti hiyo imetokana na  mahojiano zaidi ya 100  yaliyofanyika baada ya kuzimwa kwa saa 48 kwa mawasiliano kote nchini, kulikotekelezwa na mamlaka ya kijeshi ya Taliban kati ya tarehe 29 Septemba na 1 Oktoba 2025.

Laurence ameeleza kwamba madhara ya kibinadamu zilizorekodiwa ni pamoja na:

  • Kucheleweshwa au kukosa huduma za afya na dharura
  • Kuvurugika kwa shughuli za mashirika ya kibinadamu.
  • Kuongezeka kwa vizuizi vya kibaguzi dhidi ya wanawake na wasichana
  • Kukiukwa kwa maisha ya kila siku ya watu kutokana na kushindwa kuwasiliana na
  • Kuporomoka kwa shughuli za biashara na huduma za benki.       

Wanawake washindwa kuwasiliana na walezi wao wa kiume (mahram)

Ripoti inasema Wanawake na wasichana nchini Afghanistan tayari wamewekewa vizuizi vikali zaidi duniani. Wengi walioshiriki mahojiano wameeleza jinsi maisha yao yalivyokuwa magumu zaidi wakati wa kuzimwa kwa mawasiliano.

Mathalani baadhi ya wanawake wakati wa kipindi hicho walishindwa kuwasiliana na walezi wao wa kiume au kwa kilugha cha Afghanistani, mahram. Mmoja wa wanawake walioohojiwa amesema, Niliogopa sana nilipokuwa nikitembea kurudi nyumbani peke yangu, lakini kwa bahati nzuri nilifika salama baada ya saa moja.”

Kwa mujibu wa sheria za sasa za mamlaka hizo, wanawake lazima waandamane na walezi hao au mahram  wanaposafiri zaidi ya kilomita 78, au hata wanapoenda kufanya kazi, kununua bidhaa, au kupata huduma za afya katika baadhi ya maeneo.

Pia, elimu mtandaoni ndiyo njia pekee iliyosalia kwa wasichana wengi wa Afghanistan kuendelea na masomo, kufuatia marufuku ya mamlaka hizo dhidi ya elimu ya juu kwa wasichana baada ya darasa la sita.

Zile zilikuwa siku na usiku mgumu sana kwetu. Tulihofia kurudishwa kwenye enzi za mawe za historia ya binadamu. Ilikuwa kipindi cha mateso makubwa maishani mwangu.” Mwanafunzi mmoja amesema: 

Madhara katika huduma za afya

Wahudumu wa afya wameripoti vifo ambavyo vingeelezeka kama vilivyoweza kuzuilika kutokana na kukosekana kwa mawasiliano.

Muuguzi mmoja amesema  mwanamke mjamzito katika mkoa wa Laghman alipoteza mtoto wake kwa sababu gari la wagonjwa lililohitajika halikuweza kupatikana, kutokana na mfumo wa simu kuwa umekatika.

“Kama mhudumu wa afya, nimefundishwa kuokoa maisha, lakini bila mawasiliano nilijihisi mnyonge kabisa,” amenukuu msemaji wa OHCHR.  

Mashirika ya kibinadamu yameripoti kuwa kuzimwa huko kuliathiri vibaya kazi zao na kuchelewesha utoaji wa misaada kwa watu waliokuwa na mahitaji makubwa, hasa waliokuwa wakihitaji msaada kufuatia tetemeko la ardhi la tarehe 31 Agosti 2025 lililokumba mikoa ya Nangarhar, Laghman, na Kunar, pamoja na  wahamiaji waliorejeshwa kwa lazima kutoka Pakistan.

Kuzimwa kwa mawasiliano na vizuizi visivyo vya uwiano vinakiuka haki za uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa habari, na havilingani na wajibu wa Afghanistan chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.” Amesema Laurence.

Wito kwa mamlaka za Afghanistan

Hadi sasa, mamlaka za kijeshi nchini Afghanistan hazijatoa tamko lolote kuhusu sababu za kuzimwa kwa mawasiliano.

OHCHR inazitaka kutimiza wajibu wao kama walinzi wa haki za binadamu, na kuhakikisha kwamba vizuizi vyovyote dhidi ya uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa habari vinazingatia sheria, ni vya lazima, na vina uwiano sahihi na sababu halali chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *